ABIRIA SGR KUPIMA MOYO BURE
Abiria wanaosafiri kwa treni ya kisasa ya SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma watanufaika na huduma za uchunguzi na vipimo vya afya ya moyo bila malipo, baada ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Hayo yamesemwa leo Septemba 18, 2026, katika Stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa JKCI, Dkt. Peter Kissenge, aliyesema huduma hizo zitatolewa kuanzia Septemba 21 hadi 27, mwaka huu.
Amesema katika kipindi hicho, wataalamu na mabingwa wa afya watasafiri ndani ya treni ya SGR kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza kwa abiria watakaohitaji.
Dkt. Kissenge amesema huduma hizo zitatolewa bure kuelekea maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani inayofanyika Septemba 29 kila mwaka.
“Vipimo hivi vyote vikiwemo Echo, ECG, vipimo vya sukari na mafuta kwenye damu vikitolewa hospitalini vinaweza kugharimu zaidi ya Shilingi 500,000, lakini kwa kipindi hiki chote cha wiki ya afya ya moyo, abiria wote watapata huduma hizi bure kabisa wakiwa safarini,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Masanja Machibya, amesema ushirikiano huo ni mwanzo wa mpango mkubwa zaidi wa kimkakati kati ya TRC na JKCI.
Amesema TRC ipo katika hatua za usanifu wa kutengeneza mabehewa maalumu yatakayokuwa na vifaa vya matibabu na vitanda kwa ajili ya kuwasafirisha wagonjwa mahututi na wanaopewa rufaa kutoka mikoani kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa haraka na usalama zaidi.
“Mabehewa haya yatasaidia sana kupunguza muda wa kusafirisha wagonjwa waliopo kwenye hali mbaya kutoka mikoani kama Dodoma na Morogoro kulinganisha na kutumia magari ya dharura (ambulance) ya barabarani,” amesema.
Ameongeza kuwa mpango huo wa mabehewa ya matibabu unatarajiwa kuanza kufanya kazi ndani ya miezi sita ijayo, huku akiwataka wananchi na abiria wote watakaosafiri na SGR katika wiki hiyo kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo kupima na kuchunguza afya zao.

No comments
Post a Comment