Zinazobamba

MTUHUMIWA WA UNYANG'ANYI APIGWA RISASI UBUNGO

DAR ES SALAAM.

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemjeruhi kwa risasi mtuhumiwa wa unyang’anyi baada ya kukaidi amri ya kukamatwa na kuonesha vitendo vya kutaka kumdhuru askari kwa kutumia panga.

Tukio hilo limetokea Septemba 15, 2026 saa 6:50 mchana katika eneo la Kibo Makaburini, pembezoni mwa Mto Gide, Ubungo, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, mtuhumiwa huyo ametambuliwa kwa jina la Yusuph Ibrahim Mwakasamala ‘Arego’, mwenye umri wa miaka 22, mkazi wa Kimara Matosa, Wilaya ya Ubungo.

Polisi imesema mtuhumiwa huyo alijeruhiwa kwa risasi katika nyonga na mkononi baada ya kujaribu kumdhuru askari kwa panga, hatua iliyosababisha askari kujihami.

Watuhumiwa wengine wawili waliokuwa katika tukio hilo walifanikiwa kutoroka.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa huyo aliwahi kuhusishwa na matukio ya unyang’anyi wa pikipiki kwa kutumia mapanga na pia aliwahi kufikishwa mahakamani mwaka 2025 kwa tuhuma za kihalifu.

Katika tukio hilo, Polisi imekamata pikipiki yenye namba za usajili MC 809 FAV aina ya Boxer nyeusi, pamoja na panga, visu viwili na bastola bandia vinavyodaiwa kuwa mali ya mtuhumiwa.

Mtuhumiwa amepelekwa hospitalini kwa ajili ya matibabu na hali yake imeelezwa kuwa si nzuri. Polisi imesema hatua za kisheria dhidi yake zitaendelea baada ya matibabu.

Wakati huo huo, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imesema imemkamata na kumuhoji mtu mmoja anayedaiwa kuhusika na taharuki iliyotokea katika Uwanja wa Azam Complex wakati wa mchezo kati ya Yanga na Gaborone ya Botswana.

Jeshi la Polisi limesema hali ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla ni shwari na litaendelea kushirikiana na wadau wengine wa usalama kuhakikisha hali hiyo inaendelea.

No comments