Zinazobamba

NYANDUGA: MARIDHIANO HAYAWEZI BILA UKWELI WA YALIYOTOKEA OKTOBA 29,2025


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Tom Nyanduga, amesema Tanzania inahitaji kukabiliana na changamoto za mauaji, watu kupotea na kutekwa pamoja na mapungufu ya mifumo ya uchaguzi kuelekea chaguzi zijazo.

Kauli hiyo ameitoa leo, Septemba 15, 2026, jijini Dar es Salaam, katika mkutano wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Demokrasia ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Nyanduga amesema Siku ya Kimataifa ya Demokrasia inatoa fursa ya kutathmini hali ya demokrasia nchini, hasa mauaji yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata.

Amesema mauaji yaliyotokea katika kipindi hicho yameacha majeraha ambayo bado hayajapona, huku akisisitiza kuwa Tanzania haiwezi kuingia katika chaguzi nyingine bila kutafakari kwa kina yaliyotokea na kuchukua hatua ili yasijirudie.

“Tunaposema demokrasia ya Tanzania iwe demokrasia halisi na endelevu, haya matatizo lazima yakomeshwe ili yasijirudie katika chaguzi zijazo,” amesema Nyanduga.

Nyanduga amesema hatua hiyo inahitaji kutambua kilichotokea, kukubali ukweli wa matatizo hayo na kubaini waliohusika kupitia uchunguzi unaoaminika na unaohusisha wadau mbalimbali.

Amesema majadiliano hayo yanapaswa kuhusisha Serikali, makundi mbalimbali, wahanga pamoja na ndugu za watu walioathirika na vurugu na mauaji, ili hatua za uwajibikaji zichukuliwe na kujenga msingi wa maridhiano.

Amesema pia kuna haja ya kuimarisha mfumo wa uendeshaji wa uchaguzi na mifumo ya uwajibikaji, akisema ingawa mambo hayo yameainishwa katika Katiba na sheria, bado kuna mapungufu katika utekelezaji wake.Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, amesema demokrasia haiishii kwenye uchaguzi pekee, bali inahusisha utawala wa sheria, uhuru wa kujieleza, haki za binadamu, kupata taarifa na uhuru wa vyombo vya habari.

Amesema wananchi wanapaswa kutambua kuwa uhuru wa kupata taarifa na kujieleza ni sehemu ya demokrasia, hivyo kila siku inapaswa kuwa siku ya kulinda na kufurahia uhuru huo.

Henga amesema hali ya demokrasia nchini bado ina changamoto, akitaja watu kupoteza ndugu zao, wengine kutokujulikana walipo na baadhi kuwa magerezani kutokana na masuala yanayohusiana na siasa.

Amesema changamoto hizo zinaonekana pia katika utekelezaji wa sheria, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kutoa maoni, akisema kuna watu wamekuwa wakikamatwa kutokana na maoni wanayotoa kwenye mitandao ya kijamii.

“Bado hali ya demokrasia siyo nzuri sana nchini kwetu (Tanzania), ndiyo maana tuliweka hii Kongamano tujadili pamoja, tuone tunatoka wapi na tunakwenda wapi,” amesema Henga.

Hata hivyo, ametaka mazungumzo yaendelee na kutoa wito kwa Serikali kuangalia mkataba wa Afrika kuhusu haki za kidemokrasia, huku akisisitiza pia umuhimu wa kuendelea na mjadala wa Katiba mpya.

Amesema Katiba mpya haiwezi kuwa suluhisho la kila tatizo, lakini inaweza kusaidia kufungua njia ya kushughulikia sehemu kubwa ya changamoto zilizopo.Naye Katibu Mkuu Shura ya Maimamu Tanzania Sheikh Ponda Issa Ponda, amesema makongamano hayo ni muhimu katika kutafakari hali ya nchi na kutafuta namna ya kutoka katika mazingira magumu ya kisiasa na kiusalama yaliyopo.

Sheikh Ponda amesema demokrasia inagusa maisha ya wananchi kwa upana na si masuala ya kisiasa pekee, akisema mjadala kuhusu Katiba umeonyesha kuwepo kwa mitazamo tofauti ndani ya jamii.

Ponda amesema kuna kundi linalotaka mchakato wa Katiba mpya uliowahi kuanza uendelee, huku akitaja Chadema na ACT-Wazalendo miongoni mwa wanaounga mkono msimamo huo.

Amesema kundi jingine linaona kuwa kwa sasa marekebisho ya Katiba iliyopo yanaweza kutosha, wakati kundi la tatu limeibuka na kupendekeza Katiba ya mpito kabla ya baadaye kupatikana Katiba mpya.

Amesema pia wananchi wana mitazamo tofauti kuhusu Katiba mpya, hali inayofanya iwe muhimu kutafuta namna ya kuwakutanisha watu katika meza moja ya majadiliano.“Ni lazima tutafute namna ya kuja kuwaleta watu pamoja tena katika majadiliano,” amesema Sheikh Ponda.

Amesema suala la maridhiano haliwezi kutenganishwa na maumivu yaliyowapata wananchi na familia zao, akisema watu wameuawa na wengine kupotea huku familia zao zikiendelea kubeba maumivu.

Ametoa mfano wa tukio la Oktoba 16, 2017 katika msikiti mmoja wa Hijra, akisema watu waliovaa mavazi yanayofanana na ya Jeshi la Polisi waliingia msikitini na kuwachukua watu wanne waliokuwa kwenye kikao cha kamati ya msikiti.

Amesema watu hao hadi sasa hawajulikani walipo, akisisitiza kuwa masuala kama hayo yanapaswa kuzingatiwa katika mchakato wa maridhiano.

“Unapofikiria kule unataka kuleta sasa hali ya ubinadamu, hali ya pamoja na mshikamano, lazima mambo kama haya yazingatiwe yote, yatatuliwe na yapatiwe ufumbuzi,” amesema.

Amesema vikao hivyo vinawakutanisha wawakilishi kutoka makundi mbalimbali, wakiwamo viongozi wa dini, ili kila kundi liwasilishe hoja zake na hatimaye kufikia muafaka wa kitaifa.



No comments