TTCL HAKIKISHENI MNAFIKISHA FAIBA KATIKA NYUMBA ZAIDI YA MILIONI MOJA IFIKAPO 2028: WAZIRI KAIRUKI.
Na Mwandishi Wetu:Dar es salaam.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, ameliagiza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuongeza kasi ya uunganishaji wa huduma ya intaneti ya mkongo wa nyuzi majumbani (Fiber to the Home – FTTH) ili kufikisha huduma hiyo katika nyumba milioni moja ifikapo Juni 2028.
Kairuki ametoa agizo hilo leo,Agost 21, 2026, jijini Dar es Salaam,wakati akizindua rasmi awamu ya pili ya mradi wa “Faiba Mlangoni Kwako”, unaotekelezwa na TTCL kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa intaneti yenye kasi,ubora na uhakika kwa wananchi,taasisi na wafanyabiashara Tanzania bara na Zanzibar

Waziri huyo amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha uchumi wa kidijitali,kwa kuwa intaneti ya kasi inawawezesha wananchi kupata fursa za elimu, ajira, biashara, ubunifu na huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
“Faiba si waya tu unaofika nyumbani au ofisini,bali ni daraja muhimu linalomuunganisha mwananchi na fursa za uchumi wa kidijitali,” amesema Waziri Kairuki.
Nakuongeza "Watumiaji wa faiba bado ni wachache ambapo takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa robo mwaka iliyoishia Juni 2026 zinaonyesha kuwa usajili wa intaneti nchini ulifikia milioni 62.7, huku matumizi ya data yakifikia petabytes 1,041.
Hata hivyo,amesema watumiaji wa huduma ya faiba majumbani walikuwa 178,904 pekee, hali inayoonyesha bado kuna pengo kubwa kati ya mahitaji ya intaneti na upatikanaji wa huduma ya faiba kwa kaya.
Kairuki amesema awamu ya pili inalenga kuongeza wigo wa huduma hiyo hadi kufikia home passes laki Tano(500,000,) kabla ya kufikisha milioni moja ifikapo Juni 2028.
Amesisitiza kuwa mafanikio ya mradi hayapaswi kupimwa kwa idadi ya nyumba ambazo faiba imepita pekee,bali pia kwa idadi ya wateja wanaounganishwa,ubora wa huduma,kasi halisi ya intaneti, muda wa kutatua hitilafu,gharama na kuridhika kwa wateja.
“Hatupaswi kuridhika na faiba kupita mbele ya nyumba ikiwa kaya haiwezi kujiunga,hatupaswi kuridhika na usajili ikiwa huduma haitimizi ahadi ya kasi na uhakika,” amesema.
Halikadhalika ameitaka TTCL kupanua huduma hiyo katika maeneo yanayokua kwa kasi,vituo vya biashara,masoko,maeneo ya viwanda, shule, vyuo, vituo vya afya na ofisi za Serikali Tanzania bara na Zanzibar.

Pia amelitaka shirika hilo kurahisisha taratibu za usajili na kupunguza muda wa kuunganisha huduma.
Aidha amesema TTCL inapaswa kushirikiana na serikali za mitaa, waendelezaji wa makazi, wamiliki wa majengo na jumuiya za wafanyabiashara ili kuongeza idadi ya wananchi wanaotumia huduma ya faiba.
Katika kuboresha huduma kwa wateja, Kairuki ameitaka TTCL kuimarisha ufuatiliaji wa mtandao, matengenezo ya kinga na urejeshaji wa huduma kwa haraka pale hitilafu zinapotokea.
Amesema mteja hapaswi kulazimika kufuatilia mwenyewe tatizo aliloripoti,bali TTCL inapaswa kumjulisha hatua zilizofikiwa na kuhakikisha changamoto yake inatatuliwa kwa wakati.
Pia ameitaka TTCL kubuni vifurushi vinavyoweza kumudu kaya na makundi mbalimbali,wakiwemo wanafunzi,vijana, wafanyakazi,wavuvi,wachimbaji, wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na taasisi.
Amesisitiza kuwa gharama za kuunganisha huduma,vifaa na vifurushi hazipaswi kuwa kikwazo kwa wananchi.
Aidha, ameitaka TTCL kusimamia kwa karibu wakandarasi na wazabuni wanaotekeleza miradi hiyo ili kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati,kwa ubora na kwa kuzingatia mikataba.
Kairuki amesema madhumuni ya Serikali ni kuona TTCL ikiwa na zaidi ya wateja milioni mbili hadi milioni tatu wanaotumia huduma za faiba majumbani ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Abubakar Asenga, ameishauri Serikali kuongeza uwekezaji na bajeti kwa TTCL ili kuwezesha upanuzi zaidi wa huduma za intaneti.
Asenga amesema Bunge kupitia Kamati hiyo limekuwa likisisitiza kwa miaka kadhaa umuhimu wa kuimarisha TTCL ili iweze kuwa chombo muhimu katika kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi na kuongeza mapato ya Taifa.
Amesema hadi mwaka wa fedha 2024/25, TTCL ilikusanya takribani Sh bilioni 100 kupitia kuunganisha wateja wapatao 280,000.
Mwenyekiti huyo amesema lengo la mpango huo ni kufikisha mapato ya takribani Sh bilioni 400 ifikapo mwaka 2029 baada ya kuunganisha wateja zaidi ya milioni moja,huku idadi ya wateja milioni mbili ikiweza kulifikisha shirika kwenye mapato yanayokaribia Tsh. trilioni moja ifikapo mwaka 2030.
Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, amesema awamu ya pili ya mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kibiashara wa miaka 10 wa shirika hilo unaoanzia mwaka 2025/26 hadi 2034/35,kwa ajili ya kujenga home pass laki nne(400,000).
Marwa amesema TTCL imeanza kutumia teknolojia ya kisasa ya GPON, inayowezesha kutoa intaneti yenye kasi kubwa,kuunganisha wateja wengi kwa wakati mmoja,kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha ubora wa huduma ikilinganishwa na teknolojia ya Point-to-Point.
Amesema awamu ya kwanza ya mradi ilitekelezwa katika maeneo ya kimkakati ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Geita, Iringa, Mbeya, Mwanza na Unguja Zanzibar, ambapo takribani home pass elfu thelathini na nane(38,000)zilijengwa.
Marwa amesema kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya intaneti, awamu ya pili ilianza Julai 2026 na inalenga kujenga jumla ya home pass laki nne(400,000) katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Amesema mpango huo utawezesha takribani maunganisho laki saba na elfu hamsini (750,000) kufikiwa ifikapo Juni 2027, huku TTCL ikiwa na mpango wa kufikisha maunganisho takribani milioni moja ifikapo Juni 2028.
Amesema utekelezaji wa mradi huo utaongeza matumizi ya teknolojia ya kidijitali na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali nchini.













No comments
Post a Comment