VIONGOZI WA JIJI LA DAR ES SALAAM WAFURAHISHWA NA MATOKEO CHANYA YA MIKOPO YA ASILIMIA 10 YA HALMASHAURI
Meye wa Jiji la Dar es salaam Nurdin Bilali(SHETTA)amesema kuwa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji hilo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu imeanza kuonesha matokeo baada ya baadhi ya wanufaika kutumia fedha hizo kuanzisha viwanda vidogo na kupanua uzalishaji wa bidhaa zao.
Meya huyo amesema hayo leo Julai 9,2026 wakati wa ziara ya viongozi wa Wilaya ya Ilala na Halmashauri ya Jiji waliotembelea mabanda ya wajasiriamali wanaoshiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba)
Aidha amesema kuwa baadhi ya vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo vimeweza kupiga hatua kubwa kiuchumi,huku vingine vikifikia hatua ya kuanzisha viwanda vidogo baada ya kupata fedha za kuwawezesha kuongeza uzalishaji.
“Leo tumeshuhudia kuna vikundi pale vimeanzisha viwanda vidogo vidogo na vimepata zaidi ya Sh milioni 80 za kuendelea,wengine wamepata milioni 30 na huu ni mfano tu, wapo wengi wa aina hii kwenye Halmashauri yetu,”amesema Bilali
Nakuongeza kuwa"mafanikio haya yanaonesha kuwa mikopo hiyo si suala la maneno pekee bali ni chachu ya kuwawezesha wananchi kujenga shughuli zao za kiuchumi."
Nae Mkuu wa Wilaya ya Ilala,Edward Mpogolo,amesema ziara hiyo imetoa fursa kwa viongozi kuona utekelezaji wa programu za uwezeshaji wananchi kupitia mikopo ya halmashauri.
Amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetenga zaidi ya Sh bilioni 22 kwa ajili ya mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali,huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kukuza biashara na uzalishaji wao.
"Bidhaa zilizooneshwa na wajasiriamali katika maonesho hayo zimeonesha ubora mkubwa na zina uwezo wa kushindana na bidhaa kutoka nje ya nchi."amesema DC Mpogolo
Nakuongeza kuwa"Tumeona bidhaa ambazo unaweza kuzipeleka supermarket yoyote na zikashindana na biashara yoyote au bidhaa yoyote kutoka nje ya Tanzania,hivyo tutaendelea kushirikiana na wajasiriamali hawa ili kufikia lengo la Serikali la kuwainua kiuchumi".
Aidha amefafanua kwamba Serikali imeendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha Watanzania kupitia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050,ambapo kila mwananchi anapaswa kuwa na nafasi ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam Elihuruma Mabelya amesema kuwa Jiji la Dar es salaam limetumia Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kujifunza mbinu zitakazosaidia kuboresha utoaji wa huduma za ardhi,kupunguza migogoro ya umiliki na kurahisisha upatikanaji wa hati kwa wananchi.
Amesema kuwa kupitia ziara hiyo imetoa fursa kuwa kwa viongozi hao kujionea huduma zinazotolewa na Wizara ya Ardhi pamoja na kazi inayofanywa na watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kuwahudumia wananchi.
Mabelya amesema kupitia banda hilo wamejifunza umuhimu wa kuwa na kituo cha pamoja cha utoaji wa huduma za ardhi kitakachorahisisha upatikanaji wa hati,leseni za makazi, ulipaji wa kodi ya ardhi pamoja na huduma nyingine zinazohusu sekta hiyo.
"Kituo cha pamoja cha huduma za ardhi kinaweza kutusaidia kupunguza malalamiko ya wananchi na changamoto wanazokutana nazo katika utoaji wa hati, leseni za makazi na huduma nyingine za ardhi," amesema Mabelya 

Amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itatumia mafunzo yaliyopatikana katika maonesho hayo kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuongeza ufanisi katika kushughulikia masuala ya ardhi.
Amesema halmashauri itashirikiana na Wizara ya Ardhi kupitia maelekezo ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala,kufuatilia changamoto za urasimishaji wa makazi, ikiwemo kupitia kampuni ambazo hazijatimiza wajibu wake ili kuharakisha utekelezaji wa zoezi hilo.
"Maonesho haya si tu yanatoa huduma kwa wananchi, bali yanatupa dira ya namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma katika sekta ya ardhi,"amesema
Akielezea kuhusu migogoro ya ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam,Mabelya amesema migogoro mingi inaanzia ndani ya familia kutokana na kukosekana kwa uwazi katika umiliki wa mali.

Amesema familia zinapaswa kushirikishana kuhusu umiliki wa ardhi na mali nyingine ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza baadaye kati ya wanandoa, watoto au ndugu.
Hata hivyo viongozi hao wametoa wito kwa wananchi kutumia huduma zinazotolewa katika banda la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwemo elimu kuhusu mikopo, pamoja na huduma za ardhi ambapo hati 2,508 zimetolewa na wananchi 430 wamejitokeza kuzichukua.





No comments
Post a Comment