WAKONGO WAISHIO TANZANIA KUSHEREHEKEA MIAKA 66 YA UHURU WA TAIFA LAO, WAMPA KONGOLE RAIS SAMIA KULINDA USALAMA WAO
Na Mussa Augustine
Jumuiya ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wanaoishi nchini Tanzania wanatarajia kuadhimisha miaka 66 ya uhuru wa taifa hilo huku wakimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kudumisha usalama wao.
Akizungumza leo Juni 26, 2026, na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, rais wa jumuiya hiyo, Jean Paul Lengos-VIP, amesema maadhimisho hayo yatafanyika Juni 30 mwaka huu katika Ukumbi wa Montana uliopo Makumbusho, Wilaya ya Kinondoni, huku yakitarajiwa kuhudhuriwa na wasanii mbalimbali wa dansi kutoka DRC pamoja na viongozi wa Serikali.
"Leo tupo hapa kuongea na waandishi wa habari kwa sababu moja tu, ni kuwatangazia raia wa nchi yetu ya Kongo pamoja na Tanzania kuwa tarehe 30 mwezi huu wa Juni tutasherehekea miaka 66 ya uhuru wa Taifa letu la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hivyo tunaomba wajitokeze tusherehekee kwa pamoja," amesema.
Ameongeza kuwa, "Sherehe hizo hufanyika kila mwaka, na siku za nyuma zimefanyika katika kumbi mbalimbali ikiwemo Warehouse Masaki, lakini kwa mwaka huu tutazifanyia hapa Montana Makumbusho. Wanamuziki mbalimbali watakuwepo."
Aidha, Paul amesema kuwa umoja huo wa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waishio Tanzania unamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwalinda, kwani wanajisikia kama wapo nyumbani kwao, DRC.

Pia, umoja huo umemshukuru Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, ambaye amekuwa akiwalinda vyema diaspora wa Kongo, na kwamba wataendelea kushirikiana naye katika kuhubiri amani nchini humo, ambayo imekumbwa na machafuko ya kivita kwa muda mrefu sasa.
Aidha, amesema kuwa kiingilio cha sherehe hizo ni shilingi 30,000 za Kitanzania (TSh 30,000/=) kwa mtu mmoja ili kiwe rafiki kwa watu wengi kujumuika katika tukio hilo muhimu, hususan kwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waishio nchini Tanzania.

No comments
Post a Comment