Zinazobamba

MADIWANI KATAVI WAAHIDI KULINDA MIUNDOMBINU YA UMEME


Madiwani wa Halmashauri Madiwani Manispaa ya Mpanda na Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo Mkoani Katavi wamesema kwa kushirikiana na Wananchi, watahakikisha wanailinda miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania TANESCO iliyopo Mkoani Katavi kwa nguvu zote ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme bila vikwazo vyoyote.

Wamesema hayo Juni 27, 2026 walipotembelea Bwawa la Kufua Umeme wa Maji la Julius Nyerere lililopo  katika eneo la  Mikoa mitatu ya  Pwani, Morogoro na Lindi na kujionea utekelezaji wake uliofanywa na Serikali huku wakisema Bwawa hilo ndio uchumi wa nchi na kuwa uzalendo wa hali ya juu unahitajika kulilinda.Wamesema Serikali ya Awamu ya sita imewekeza kwa nguvu zote fedha nyingi na juhudi kubwa katika kukamilisha ujenzi wa Bwawa hilo na kuwa wananchi wote wa Tanzania wana deni kwa Serikali katika kuhakikisha wanailinda miundombinu ya umeme ya TANESCO ili kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali kupitia Taasisi yake ya TANESCO.Akizungumza kwa Niaba ya Madiwani, Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mpanda Mhe. Nuru Abdalah amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, anastahili pongezi za kipekee kwa namna alivyohakikisha ndoto ya Tanzania ya kuwa na Bwala hili lenye uwezo wa kuzalisha umeme  megawati 2115  inakamilika na watanzania kufurahia fursa mbalimbali za upatikanaji wa umeme wa uhakika ambao ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa nchi na wa mtu mmoja mmoja.Ameongeza kuwa, Mkoa wa Katavi, unampongeza  Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO Bw. Lazaro Twange, katika utendaji kazi wake na namna anavyotumia hekima kubwa katika suala zima la ushirikishwaji wa viongozi na wananchi kupata uelewa wa kazi kubwa inayofanywa na TANESCO katika kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi na wateja wake wote kiujumla.

“Nimeona namna ambayo Serikali chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya kazi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika, tulichokiana hapa sasa tunakwenda kuwaelezea wananchi wetu umuhimu wa mradi huu, na jinsi ya kuutuza ili uweze kutumika kwa muda mrefu”.

Ameahidi kwa niaba ya timu nzima ya viongozi kutoka mkoa wa Katavi waliotembelea Bwawa hilo, kuwa mabalozi wazuri wa TANESCO katika suala zima la Ulinzi wa Miundombinu ya Umeme.Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara hiyo, Meneja wa Bwawa la Umeme wa Maji la Julius Nyerere na Miundombinu Mha. Erick Mwageni amewaomba viongozi hao kuendelea kuhamasisha suala la ulinzi wa Miundombinu ya TANESCO Mkoani Katavi,  ili kuhakikisha miundombinu ya umeme mkoani humo inakuwa salama kwani walinzi nambari moja wa miundombinu ya TANESCO ni wananchi wenyewe wanaoishi jirani na miundombinu hiyo ya umeme.“Leo  tumetembelewa  na  waheshimiwa Madiwani pamoja na viongozi mbalimbali  kutoka Mkoa wa Katavi  katika ziara yao wamekuja  kujionea uwekezaji  mkubwa  ambao  umefanywa na Serikali katika mradi  huu wa kuzalisha umeme wa JNHPP, pamoja  na  kuona  shughuli  mbalimbali tunazozifanya kama TANESCO  baada  ya kukamilika  kwa asilimia 100 ya ujenzi wa  mradi huu”.



No comments