UPATIKANAJI UMEME KUENDELEA KUIMARIKA MKOANI IRINGA— MHE. SALOME

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Iringa.
Amesema tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, Mkoa wa Iringa umepokea zaidi ya shilingi bilioni 124 kwa ajili ya kuimarisha huduma ya umeme na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma hiyo kwa lengo la kuwawezesha kujiletea maendeleo ya kiuchumi.
Mhe. Salome ameyasema hayo leo Mei 23, 2026 wakati akijibu hoja za wananchi mkoani Iringa, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.
Amesema changamoto za umeme zilizokuwa zikikabili baadhi ya maeneo ikiwemo Kata ya Mafifi tayari zimeshapatiwa ufumbuzi na wananchi wanaendelea kupata huduma ya umeme wa uhakika. Hata hivyo, amesema katika Mtaa wa Mosi huduma hiyo bado haijafika ipasavyo ambapo tayari maelekezo yametolewa kwa TANESCO na REA kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanaunganishiwa umeme kwa wakati.
Pia ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya wananchi kuunganishiwa umeme kwa gharama nafuu ya shilingi elfu 27,000 tu, huku akielekeza kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya mjini lakini kiuhalisia wanaishi mazingira ya vijijini waunganishiwe umeme kwa gharama hiyo pia.
Katika kuimarisha zaidi huduma ya umeme mkoani Iringa, amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendelea kuongeza uwezo wa Kituo cha Kupokea na Kusambaza Umeme cha Mufindi ambapo Mkoa huo utaanza kupata umeme kutoka megawati 60 hadi megawati 260.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kubadilisha transfoma katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji ili kuwezesha viwanda kufanya kazi muda wote na wananchi kuendelea kupata umeme wa uhakika.
Sambamba na hayo, Mhe. Salome amesisitiza umuhimu wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa ili kulinda mazingira na kuboresha afya na maisha ya wananchi. Amesema Serikali inaendelea kutoa ruzuku ya majiko ya gesi na majiko banifu kwa wananchi wa vijijini na kuwahamasisha kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.



No comments
Post a Comment