TAMASHA LA 'KEKO BILA UHARIFU INAWEZEKANA' KUZINDULIWA MEI 29,2026
Na Mussa Augustine.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mh.Sixtus Mapunda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Tamasha la “Keko Bila Uhalifu Inawezekana”, lililoandaliwa na Diwani wa kata ya Keko, Ismail Saidi Amanzi, kwa lengo la kusaka na kuinua vipaji vya vijana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mapema leo Mei 28, 2026, wakati wa zoezi la kupima uzito kwa mabondia watakaopanda ulingoni kesho, Diwani Amanzi amesema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika huku akiwaomba wadau na wananchi kujitokeza kwa wingi.
“Hili tamasha limebeba michezo mbalimbali. Kutakuwepo muziki wa singeli, ngoma za asili, maigizo na mchezo wa ngumi. Kila kundi kutakuwa na mshindi wa kwanza na wa pili ambao watapata zawadi kama ilivyopangwa,” amesema Amanzi.
Aidha, amesema kuwa lengo la tamasha hilo ni kuondoa vitendo vya uhalifu kutokana na kata hiyo kusifika kwa vitendo hivyo, pamoja na kuinua vipaji vya vijana.
Amesema kuwa Serikali ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imeanzisha Wizara ya Maendeleo ya Vijana kwa lengo la kuondoa changamoto zinazowakabili vijana, hivyo yeye kama diwani wa kata hiyo amekuwa mstari wa mbele kusimama na vijana katika kuinua vipaji ili kupata wachezaji wa kitaifa na kimataifa.
“Mimi kama diwani ni mmoja wa mfano. Nimeandaa tamasha na ulingo wa kufanyia pambano la ngumi, nimefungua studio kwa lengo la kuendeleza muziki. Nataka vijana wailinde Keko yao wenyewe. Nitakuwa pamoja nao katika shida na raha.”
Aidha, amesema viongozi mbalimbali watakuwepo, akiwemo Naibu Meya wa Temeke pamoja na madiwani wengine, kushuhudia tamasha hilo la aina yake.
Kwa upande wake, Polisi Kata ya Keko, Insp. Sospeter Antipus Oyuke, amesema kuwa tamasha hilo lenye lengo la kuzuia uhalifu litafanyika kwa amani kwani suala la ulinzi limeimarishwa.
“Tunawakaribisha sana wananchi kwani ulinzi na usalama umeimarishwa. Hakutakuwa na changamoto ya aina yoyote,” amesema Insp. Oyuke.
Naye refa wa michezo ya tamasha hilo, Tusajigwe Mwatonoka, amempongeza Diwani Amanzi kwa kuanzisha mapambano hayo ili kuwanusuru vijana dhidi ya vitendo vya uhalifu na kuinua vipaji vya vijana wa Keko.
“Naomba akina mama wajitokeze kwa wingi kushuhudia tamasha hili kwani diwani wetu ana dhamira ya dhati ya kuwainua vijana wetu kupitia michezo mbalimbali,” amesema Mama Rasi
Hata hivyo, mmoja wa mabondia anayefahamika kwa jina la Francis Kavishe amemshukuru Diwani Amanzi kwa kuwaletea tamasha hilo na kusema kuwa yupo tayari kupambana ili kurudisha hadhi ya Keko ambayo imekuwa ikizalisha mabondia wengi.


No comments
Post a Comment