Zinazobamba

WAZIRI SANGU AONGOZA MAADHIMISHO YA MIKA 19 YA KANISA LA WRC

Na Mwandishi Wetu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano),Deus Sangu ameongoza maadhimisho ya miaka 19 ya Kanisa la Huduma ya Neno la Upatanisho(WRC),linaloongozwa na Askofu na Nabii Nicolaus Suguye.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Aprili 6,2026 jijini Dar es Salaam,Waziri Sangu ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala,Edward Mpogolo,Mbunge wa Jimbo la Kivule Ojambi Massaburi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Bunda Ester Bulaya, ambapo walipokelewa kwa bashasha kubwa na waumini na viongozi wa kanisa hilo.

Mbali na viongozi hao,pia wamehudhuria viongozi mbalimbali wa dini akiwemo Askofu wa Kanisa la Arise & Shine,Boniphace Mwamposa na Askofu wa Kanisa la Ufunuo Tanzania,Paul Bendera.

Maadhimisho hayo yamepambwa na nyimbo za sifa na shukrani,huku waumini wakionesha furaha na kujivunia mafanikio ya kanisa lao tangu kuanzishwa kwake.Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Sangu amepongeza huduma inayotolewa na kanisa hilo,akisema imekuwa na mchango mkubwa kwa jamii.

"Tunafurahia kazi ya Mungu mnayoifanya kupitia huduma yenu,heshima hii umepewa Askofu kwa kazi kubwa uliyoifanya,” amesema.

Waziri Sangu amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini katika kuimarisha maendeleo ya jamii na kudumisha amani nchini.

Amesema taasisi za dini zimekuwa na mchango mkubwa katika malezi ya maadili pamoja na utoaji wa huduma kwa jamii.

Aidha, amewasilisha salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan,akibainisha kuwa Serikali inaendelea kuthamini mchango wa taasisi hizo katika kuleta mshikamano na maendeleo.

Ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni,taasisi za dini zimekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii kwa kutoa misaada kwa wahitaji na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Waziri huyo pia ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi hizo ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili.Kwa upande wake,Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo,akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila amewashukuru viongozi wa dini kwa mchango wao mkubwa katika kudumisha amani na utulivu Mkoani Dar es Salaam.

"Tuna kila sababu ya kuwashukuru na kumtukuza Mungu,hata tulipowahitaji walikuja bila kusita,mafanikio na utulivu tunaouona leo ni matokeo ya mchango mkubwa wa viongozi wa dini,ambao ni muhimu sana katika Mkoa huu.”amesema DC Mpogolo.Nae Askofu wa Kanisa la WRC Nabii Nicolas Suguye amebainisha kuwa kanisa hilo lina mpango wa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii,ikiwemo kujenga Shule kwa ajili ya kutoa huduma ya elimu bure kwa watoto yatima na wale waishio katika mazingira magumu.



No comments