Zinazobamba

KAIRUKI: SEKTA YA MAWASILIANO YAPIGA HATUA KUBWA NDANI YA SIKU 100 ZA UONGOZI WA AWAMU YA PILI YA RAIS SAMIA.


Na  Mwandishi wetu Dodoma 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Angela Kairuki, amesema Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeendelea kukua kwa kasi kubwa ndani ya siku 100 za utekelezaji wa kipindi cha pili cha uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, DKT. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri Kairuki alisema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo minara ya simu na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

“Takwimu zinaonesha kuwa laini za simu zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka milioni 99.3 mwezi Oktoba 2025 hadi kufikia milioni 106.9 Januari 2026, sawa na ongezeko la asilimia 7.7,” alisema Waziri Kairuki.

Aliongeza kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti imeongezeka kutoka milioni 56.3 hadi milioni 58.1 katika kipindi hicho, ongezeko sawa na asilimia 3.2. Aidha, watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea fedha kwa njia ya simu wameongezeka kutoka milioni 71.7 hadi milioni 76.5, sawa na ongezeko la asilimia 6.7.

Gharama za Mawasiliano Zabaki Nafuu

Kwa upande wa gharama za mawasiliano, Waziri Kairuki alisema Serikali imeendelea kudhibiti bei ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa gharama nafuu.

“Gharama za kupiga simu ndani ya nchi zimeendelea kubaki Shilingi 29 kwa dakika, huku wastani wa bei ya data bila kifurushi ukiendelea kuwa Shilingi 9.35 kwa MB moja,” alisema.

Alisema mwenendo huo unaashiria kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za mawasiliano na TEHAMA hususan katika maeneo ya vijijini na yale ambayo awali hayakuwa na huduma, hali inayowawezesha wananchi kupata huduma za kifedha, afya, elimu na biashara kidijitali kwa urahisi na kwa haraka.

Ushirikiano na Sekta Binafsi

Waziri Kairuki alieleza kuwa Wizara imeendelea kushirikiana kwa karibu na Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, akitolea mfano ujenzi wa minara ya mawasiliano ambapo Sekta Binafsi huchangia asilimia 60 ya gharama huku Serikali ikigharamia asilimia 40.

“Ushirikiano huu umeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano nchini,” alisema.

Mafanikio Mengine Ndani ya Siku 100

Akizungumzia mafanikio mengine, Waziri Kairuki alisema Wizara imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Katika Mwaka wa Fedha 2025/26, Wizara ilipangiwa kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 120 kupitia mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, lakini imefanikiwa kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 132, sawa na asilimia 109.9 ya lengo.

Alisema mafanikio hayo yametokana na matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato, hatua iliyoongeza ufanisi, uwazi na kupunguza upotevu wa mapato ya Serikali.

Ujenzi wa Minara Nchini

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alisema Wizara kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imekamilisha ujenzi wa minara 758 katika kata 713 nchini kwa gharama ya Shilingi bilioni 126, ambapo wananchi takribani milioni 8.5 wanatarajiwa kunufaika.

Aidha, Wizara imekamilisha kuongeza uwezo wa minara 304 kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G kwa asilimia 100.

Kuhusu ujenzi wa minara vijijini, Waziri alisema ujenzi wa minara 636 (621 ya simu na 15 ya redio) umefikia asilimia 78 ya utekelezaji, ambapo minara 371 tayari imewashwa na kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya 67,000.

Alisisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kunachangia upatikanaji wa huduma za kifedha kwa njia ya simu, biashara mtandaoni, elimu, afya pamoja na kupunguza pengo la kidijitali kati ya vijijini na mijini.

Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, mafanikio hayo yanaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga uchumi wa kidijitali na kuhakikisha maendeleo jumuishi kwa wananchi wote.

No comments