SHINGO KUJA KIVINGINE KUWASAIDIA VIJANA KUJIKWAMUA KIUCHUMI UKONGA.
Mbunge wa Jimbo la Ukonga,Bakari Shingo amesema yupo tayari kuwasaidia vijana wa Jimbo lake kwa kuwapatia mafunzo ya udereva wa bajaji na bodaboda.
Aidha amesema mafunzo hayo yameanza Desemba 3,2025, ambapo zaidi ya vijana 140 wameanza kupata mafunzo hayo ya awamu ya kwanza
Akizungumza leo Desemba 4 ,2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilicholenga kumchagua Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam,Mhe.Shingo amesema yuko tayari kushirikiana na madiwani hao katika kuleta maendeleo kwa wananchi.
Ameeleza kwamba ushirikiano huo utaleta tija katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma bora kwa jamii.
"Natarajia kutoa mafunzo kwa vijana kwa gharama za mbunge na mfuko wa Mbunge,vijana walioko katika Jimbo letu,kwa wale wasiokuwa na leseni,tunahakikisha wanapata leseni na wasiojua kabisa tunawapatia mafunzo na lengo langu ni kuwafikia vijana kati ya 600 hadi 800",amesema Mbunge huyo.
Vilevile ametangaza kuwa atashirikiana kwa karibu na baraza la madiwani pamoja na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam,Nurdin Bilali Juma katika kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo
Hata hivyo Mhe.Shingo amempongeza Mstahiki Meya huyo mpya wa Jiji la Dar es Salaam,Nurdin Bilali kwa kupata kura 48 za ndiyo kati ya kura 51 zilizopigwa,huku Naibu Meya John Mrema akipata kura 49 za ndiyo katika mchakato wa uchaguzi huo, ambao ulikutanisha vyama vya siasa CCM,Chauma na ACT Wazalendo.

No comments
Post a Comment