MWAUWASA YAZIDI KUBORESHA MFUMO WA USAMBAZAJI MAJI
Mradi mkubwa wa kuboresha mfumo wa usambazaji wa maji safi unaoendelea kutekelezwa jijini Mwanza kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) umefikia zaidi ya asilimia 35 ya utekelezaji wake, mamlaka hiyo imethibitisha.
Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa MWAUWASA, Bi. Vivian Temu, wakati wa ziara ya waandishi wa habari waliotembelea maeneo mbalimbali yanayohusiana na utekelezaji wa mradi huo.
Kwa mujibu wa Temu, ujenzi wa matenki makubwa matano ya kuhifadhia maji unaendelea kwa kasi katika maeneo ya Kagera, Fumagila, Kisesa, Nyamazobe na Usagara. Jumla ya uwezo wa matenki hayo ni kuhifadhi lita milioni 31 za maji; ambapo tenki la Kagera na Fumagila kila moja lina uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10, Kisesa na Nyamazobe lita milioni 5 kila moja, huku Usagara likiwa na uwezo wa lita milioni 1.
Mbali na ujenzi wa matenki hayo, mradi unahusisha pia ulazaji wa mtandao wa mabomba wa jumla ya kilomita 40.5, ambapo hadi sasa zaidi ya kilomita 13.7 tayari zimekamilika. Mabomba hayo yanaunganisha vituo vya kusukuma maji vinavyojengwa katika maeneo ya Sahwa na Butimba na kuyapeleka maji kwenye matenki husika.
“Mradi huu ni wa kimkakati kwa ajili ya kuondoa kabisa tatizo la upatikanaji wa maji katika maeneo ya jiji la Mwanza, hasa yale ya pembezoni na yenye miinuko mikali. Tunatarajia bomba la kupeleka maji Kisesa litakamilika ifikapo Machi 2026,” alieleza Temu.
Mradi mzima unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba 2026 na utakapohitimishwa, zaidi ya wakazi 450,000 wa jiji la Mwanza na vitongoji vyake watafaidika moja kwa moja na huduma bora ya maji safi.
Chanzo kikuu cha maji kwa mradi huu ni kituo kipya cha Butimba, ambacho nacho kinajengwa chini ya mradi huu kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD).
Akizungumzia faida za mradi huo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Bw. Waisa Werema, alisema kuwa jamii yake imeanza kuona mafanikio ya mradi, akitaja kupungua kwa uhaba wa maji kama hatua kubwa ya maendeleo. Alitoa pongezi kwa uongozi wa MWAUWASA na serikali kwa namna wanavyoshirikiana na viongozi wa mtaa kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa wakati.
Lengo kuu la mradi ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma endelevu ya maji safi kwa wakazi wa Mwanza, kuongeza uwezo wa uhifadhi wa maji, na kuboresha afya, mazingira na hali ya kiuchumi ya wananchi wa jiji hilo.
No comments
Post a Comment