Kampeni za NLD Zakoleza Moto Dodoma. Doyo Aahidi Soko Huru la Mbaazi kwa Wakulima wa Kondoa”
Kampeni za Chama cha NLD zimeendelea kupata mwamko mkubwa baada ya mgombea urais wa chama hicho, Mhe. Doyo Hassan Doyo, kufanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Stand ya Zamani, wilayani Kondoa.
Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza, Mhe. Doyo alisema moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wakulima wa mbaazi nchini ni mfumo wa stakabadhi ghalani, ambao umekuwa ukiwanyima wakulima faida stahiki. Alibainisha kuwa wakulima wanahitaji soko la uhakika litakalowaletea tija ya moja kwa moja.
“Asubuhi nilipowasili Kondoa, wazee waliniita na kuniuliza kuhusu mstakabali wa soko la mbaazi. Nimewaambia wazi kuwa iwapo watanipa kura, kura zao kwangu ni dhamana ya kuhakikisha kila mkulima anapata soko huru na la uhakika kwa asilimia 100, nitahakikisha kila mkulima anauza mbaazi kwa soko analolichagua mwenyewe, na siyo kulazimishwa kuuza kwa bei ya shilingi 400 kwa kilo kama ilivyo sasa chini ya CCM,” alisema Mhe. Doyo.
Akiendelea kuwashawishi wananchi, Doyo, alisema kuwa kilimo cha mbaazi ni sekta yenye tija kubwa kitaifa, lakini kwa sasa kilimo hicho hakijamletea mkulima wa kawaida matokeo bora ya kiuchumi. Alisisitiza kuwa kuchagua NLD ni kuchagua uhuru wa mkulima katika masoko na kipato chenye manufaa.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa NLD katika Jimbo la Kondoa, Bi. Faudhia Abdul, aliwaomba wananchi kumchagua yeye pamoja na mgombea urais wa chama hicho, akibainisha kuwa watashirikiana kutatua changamoto sugu zinazowakabili wakazi wa Kondoa, hususani upatikanaji wa maji na soko la mbaazi.
“Wilaya ya Kondoa tuna chanzo cha maji cha chemchem ambacho hakikauki kwa miezi yote 12 ya mwaka. Endapo nitaaminiwa na kuchaguliwa kuwa mbunge wenu, nitahakikisha chanzo hiki kinatumika ipasavyo ili wananchi waepukane na adha ya maji,” alisema Bi. Faudhia.
Msafara wa mgombea urais wa NLD unaelekea mkoa wa Iringa na Njombe kwa mikutano ya kampeni inayoendelea nchi nzima.
No comments
Post a Comment