Zinazobamba

DOYO AWAHIDI WAKULIMA WA NJOMBE RUZUKU, MASOKO YA UHAKIKA NA VIWANDA VYA MBAO


Njombe

Mgombea urais kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Doyo Hassan Doyo, ameendelea na kampeni zake kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu. 

Leo amefanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya soko la wakulima, Jimbo la Njombe Mjini, mkoani Njombe.

Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi, Mhe. Doyo amewahakikishia wakulima wa mkoa wa Njombe, hususan wanaojishughulisha na kilimo cha miti ya mbao, kwamba serikali yake itatoa ruzuku maalum ili kuwawezesha kuendeleza kilimo hicho, ambacho kinahitaji muda mrefu na mtaji mkubwa.

Mhe. Doyo alisema anafahamu changamoto kubwa zinazowakabili wakulima wa miti ya mbao, ikiwemo gharama kubwa za uzalishaji na muda mrefu wa kuvuna. Alisisitiza kuwa serikali yake itatoa ruzuku kuhakikisha kilimo hicho kinaendelea kwa tija na kuwa chanzo cha mapato ya uhakika kwa wananchi wa Njombe.

Aidha, Mhe. Doyo aligusia umuhimu wa kuanzishwa kwa viwanda vya mbao mkoani humo, akibainisha kuwa vitasaidia kuongeza thamani ya mazao hayo na kutoa ajira kwa vijana wengi. 

Huku akisistiza, alibainisha kuwa kupitia viwanda hivyo vya mbao, tutapata fenicha bora zinazozalishwa hapa nchini.

 Serikali yake pia itanunua fenicha kutoka viwanda vya Njombe badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi. “Tunataka fedha za Watanzania zibaki nchini na kuinua uchumi wa wakulima wetu,” alisisitiza Mhe. Doyo.

Mbali na sekta ya miti, Mhe. Doyo alisema anafahamu changamoto ya ukosefu wa soko la uhakika kwa mazao ya ngano, na akaahidi kuwatafutia wakulima masoko ya ndani na nje ya nchi, pamoja na kuvutia wawekezaji watakaowekeza katika ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuchakata ngano mkoani humo.

“Tunataka kuongeza thamani ya mazao yenu. Kupitia kiwanda cha ngano, wakulima wa Njombe watanufaika moja kwa moja badala ya kuuza mazao ghafi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa NLD, Don Waziri Mnyamani, aliwataka wananchi wa Njombe kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 29, na kumchagua Mhe. Doyo, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na mshikamano wakati wa uchaguzi.

“Wananchi wa Njombe, mstakabali wa maisha yenu uko mikononi mwenu. Nendeni mkapige kura kwa amani, mchague Doyo Hassan Doyo, muone matokeo chanya kupitia sera bora za NLD,” alisema Mnyamani.

Baada ya mkutano huo, msafara wa kampeni wa Mhe. Doyo umeelekea katika mikoa ya Songea, Lindi na Pwani kuendelea na mikutano ya kampeni katika maeneo mengine ya nchi.

No comments