ZAKAYO SHUSHU AWAHIMIZA VIJANA KUJIKITA KATIKA KUJENGA BRAND ZENYE TIJA
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Hafla ya utoaji wa Tuzo za Best Brand Africa kwa mwaka 2025 imefanyika kwa mafanikio makubwa katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Septemba 21,2025
Tukio hilo limewakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi, likiwa na lengo la kutambua na kuenzi kampuni na taasisi zilizojitofautisha katika ujenzi wa chapa imara, ubunifu wa huduma, na mchango chanya kwa jamii.
Muandaaji wa tuzo hizo, Ndg. Zakayo Shushu, alisema kuwa hafla hiyo ni mwanzo wa safari pana ya kutangaza ubora wa chapa za Kiafrika ndani na nje ya bara.
Alifafanua kuwa, ingawa tuzo zimeanzia Tanzania, azma ni kuzieneza kote barani Afrika.
"Tumeanza hapa Tanzania, lakini dhamira yetu ni kuzifikisha tuzo hizi kila kona ya Afrika. Mwaka ujao tumejipanga vizuri zaidi," alisema Zakayo Shushu mbele ya wageni waalikwa.
Tuzo hizi zimeanzishwa kwa nia ya kuonyesha hadhi ya chapa bora barani Afrika chapa ambazo zimeonesha ubora katika huduma, bidhaa zenye viwango vya juu, pamoja na uaminifu kwa wateja. Kupitia tuzo hizi, kampuni hupata kutambuliwa na kuhamasishwa kuendelea kuwekeza katika ubunifu, uboreshaji wa huduma, na mikakati ya kuimarisha chapa zao.
Katika hotuba yake, Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmon E. Mapana, alielezea kufurahishwa na juhudi za Zakayo Shushu katika kukuza sekta ya chapa.
Alimtambua Zakayo kama kijana mwenye maono makubwa na mchango wa dhati katika kukuza vipaji pamoja na taasisi za kijamii na kiuchumi.
"Zakayo amefanya kazi nzuri,tunamtambua hata alipokuwa akisaidia Madam Ritha kwenye kipindi cha BSS,hizi brand names ni muhimu na tunapaswa kuzilinda,COSOTA ipo, na haya yote ni sehemu ya kupeana moyo na kuonyesha kwamba tunaweza kufanya mambo kwa tofauti," alisema Dkt. Mapana.
Tukio hilo liliambatana na utoaji wa tuzo kwa kampuni na watu binafsi waliotambuliwa kwa mafanikio yao katika nyanja mbalimbali kama biashara, sanaa, utumishi wa umma na huduma kwa jamii.
Washindi walipokea tuzo kwa furaha, huku wakiahidi kuendeleza ubora wa huduma na kuwa mabalozi wa chapa zao.
Zakayo Shushu alihitimisha kwa kueleza kuwa tuzo za mwaka ujao zitakuwa kubwa zaidi, zikishirikisha mataifa mengi ya Afrika. Aliwahimiza wamiliki wa biashara kuzingatia ubunifu na ubora kama misingi ya kujenga chapa imara.
"Best Brand Africa si tu tuzo, bali ni harakati ya kuonyesha kuwa Afrika inaweza kujenga chapa imara zinazotambulika duniani," alisisitiza.
No comments
Post a Comment