DKT.SAMIA AVIONYA VIKAO VYA UCHUJAJI NA UTEUZI WAGOMBEA NDANI YA CCM.
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM,kupitia Mwenyekiti Taifa wa Chama hicho,Dkt. Samia Suluhu Hassan imevielekeza vikao vyote vitakavyokwenda kufanya uchujaji na uteuzi wagombea nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho viwatendee haki wagombea waliojitokeza.
Hayo yamesemwa leo Julai 3,2025 na Katibu Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Taifa Amos Makala wakati akizungumza na Waandishi wa habari ikiwa ni siku moja baada ya kukamilika kwa zoezi la kuchukua na kurejesha fomu kwa wagombea ndani ya Chama hicho katika nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia Juni 28 hadi Julai 2 Mwaka huu.
CPA Makala amesema kwamba Halmashauri Kuu Taifa ya CCM inayongozwa na Dkt.Samia haitaki kuona wagombea wanaonewa na kutengenezewa majungu na fitna katika mchakato huu wa uchujaji na uteuzi nakwamba vikao hivyo vitende haki ili kuteuwa watu wa haki.
"Tunapokwenda kwenye uchaguzi chama Cha siasa kama chama Cha Mapinduzi,tutakua na mambo ya kusema juu ya mafanikio yaliyofanywa na chama cha Mapinduzi,lakini tutakua na Ilani,hata hivyo hayo mambo yote yatanogeshwa kama tutakapokua na wagombea wazuri"amesisitiza.
Amebainisha kuwa jumla ya Wagombea wa Majimbo wapatao 4109 wamejitokeza kugombea huku kati yao wagombea 3585 ni kutoka Tanzania Bara,na wagombea 524 ni kutoka Zanzibar.
"Baada ya zoezi hili la kuchukua na kurejesha fomu kukamilika,kuanzia kesho tarehe 4,vikao vya uchujaji vinaanza katika kamati za siasa za kata,kutoa mapendekezo kwa wagombea hawa kwa ajili ya uteuzi yaani Madiwani walioomba kwenye kata,Viti maalumu,na ratiba za kamati za siasa za Mkoa zitakaa Julai 9,kwa ajili ya kufanya uteuzi wa mwisho kwa nafasi ya udiwani." Amesema
Nakuongeza kuwa" Kwa nafasi ya Uwakilishi na Ubunge ndani ya chama cha Mapinduzi uteuzi wa mwisho utafanywa na kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi mnamo Julai 19 Mwaka huu kwa maana ya wale wagombea watatu watatu."
Hata hivyo CPA Makala amewashukuru wanachama wote wa CCM na Jumuiya zake ikiwemo UWT, UVCCM na Jumuiya ya Wazizi,kwa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali zilizotangazwa na chama hicho,na kuwataka wanachama hao kuwa watulivu wakati wakisubiri zoezi la uchujaji na uteuzi wa mwisho.
No comments
Post a Comment