DKT. SAMIA MGENI RASMI MAADHIMISHO YA MIAKA 103 YA KUZALIWA HAYATI BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE.
Na Mwandishi Wetu.
Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 103 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yatakayofanyika April 13 ,2025 katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.
Taarifa hiyo imetolewa leo April 5,2025 na Mwenyekiti wa Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere Paul Petro Kimiti wakati akizungumza na vyombo vya habari Msasani Beach Jijini Dar es salaam,ambapo amebainisha kuwa maadhimisho hayo ni kumuenzi Mwalimu Nyerere kutokana na Mchango wake mkubwa kwa Tanzania, Afrika, na Duniani kwa ujumla, kwa kuwarithisha Vijana na watoto wa Taifa letu misingi Bora aliyoyaacha Nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema kuwa"Chagua Viongozi Bora kwa Ustawi wa Jamii na Maendeleo Endelevu ya Taifa," kaulimbiu ambayo inaunga mkono shughuli kubwa zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kutekeleza miradi mbali mbali ya kimkakati.
"Tukumbuke mwezi huu wa Aprili tarehe 13 ni kumbukizi ya kuzaliwa Baba wa
Taiafa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,ni siku ambayo sisi kama taasisi tunawajibu wakiitumia vizuri siku hiyo ya kumbukumbu juu ya Baba wa Taifa kwa kuenzi misingi ya Amani,Utulivu na Umoja" amesema Kimiti.
Nakuongeza kuwa" tutakua na Kongamano ambalo tumeliandaa tutalifanyia pale Dodoma tarehe 13 na 14,tunalifanya makusudi ili kushirikisha taasisi zote zinazomuenzi Baba wa Taifa lakini pia wananchi wote kuanzia Vijana wa shule za msingi wa vyuo na watu binafsi,tunaomba washiriki tuwe sote pamoja ,tena itakua jumapili siku hiyo watu waende kwenye madhehebu yao wakamuombee Baba wa Taifa kwa imani mbalimbali.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Neema Mkwachu amesema kwamba katika kuelekea siku ya kilele cha maadhimisho hayo Taasisi imeandaa wiki ya Mwalimu Nyerere itakayojumuisha ziara kwenye miradi ya kimkakati ya Taifa kwa kutembelea na kujifunza kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa Nchini.
Aidha ameongeza kuwa kutakuwa na shughuli za Mazingira kwa kupanda miti na kufanya usafi kwenye vyuo,shule, hospitali na maeneo ya umma,kwa heshima ya urithi wa Mwalimu Nyerere,pia kutakuwepo na maonyesho kuhusu mchango wa Mwalimu Nyerere katika nyanja za siasa,uchumi,Elimu,afya,utamaduni na maendeleo ya kijamii.
Halikadhalika amesema kuwa kutakuwa na Mdahalo maalumu utakaohusu umuhimu wa kuchagua viongozi Bora kwa maslahi mapana ya Taifa ikienda sanjari na maombi maalumu kwa ajili ya Taifa na mshikamano kwa Watanzania.
Nae mmoja wa wajumbe wa kamati Tendaji ya Taasisi hiyo Brigedia Mstaafu Mh.Balozi Francis Mdolwa amesema kuwa Watanzania wanaombwa siku zote kuendelea kudumisha yale mazuri yote yaliyopatikana tangu enzi za uhuru ikiwemo umoja amani na mshikamano.
Hayo ni maadhimisho ya nne tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo yenye lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere kutokana na Mchango wake mkubwa kwa Tanzania,Afrika na Dunia kwa ujumla kwa kuwarithisha Vijana na Watoto wa Taifa la Tanzania kwa misingi bora iliyoiasisiwa na kiongozi huyo enzi za uhai wake.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni