Zinazobamba

RAIS MWINYI:ZANZIBAR ITAENDELEA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA ROMANIA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar itaendelea kuimarisha Ushirikiano na Romania katika nyanja mbalimbali za Maendeleo  na Kiuchumi.

Rais Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na Balozi wa Romania nchini Tanzania , Mhe.Gentiana Serbu aliyefika Ikulu Zanzibar kuonana naye.

Aidha Rais Dkt.Mwinyi amemuelezea Balozi Gentiana kuwa  yapo Maeneo mengi ambayo hizo zinaweza kushirikiana ikiwemo Elimu , Afya, Mafuta na Gesi , Usimamizi wa Maafa na  Udhibiti wa Taka Kitaalamu pamoja na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Akizungumzia suala la Mazingira Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa  Zanzibar inakabiliwa na tatizo kubwa  la Taka  za plastiki zinazotishia Uhai wa Viumbe vya Baharini na Ustawi wa Sekta ya Utalii na kuiomba Romania kulizingatia eneo hilo.

Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amevikaribisha Vyuo Vikuu vya Romania kuja nchini kuangalia maeneo ya Ushirikiano na Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).

Vilevile ametumia fursa hiyo kuwakaribisha Wawekezaji na Wafanyabiashara wa Romania kuja kuangalia fursa za Uwekezaji Hapa nchini.Naye Balozi Gentiana Serbu ameihakikishia Zanzibar kuwa nchi hiyo itaendelea Kushirikiana nayo na kutoa Misaada katika sekta mbalimbali kwa lengo la kuleta Maendeleo na Ustawi wa Watu wake.

Balozi Gentiana ameyataja maeneo ambayo nchi yake inalenga katika Ushirikiano na Zanzibar kuwa ni  Usimamizi wa Maafa, Elimu ,Afya Teknolojia ya Mawasiliano ,Uwekezaji na Maendeleo ya Viwanda.



Hakuna maoni