Zinazobamba

TAKUKURU MKOANI PWANI YAFANYA UTAFITI KUDHIBITI RUSHWA BARABARANI.

  Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Christopher Myava

Na Mussa Augustine

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani, Christopher Myava amesema wamefanya utafiti mdogo  ili kubaini vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya askari wa Usalama barabarani Mkoani humo.

Bw.Myava ameibainisha kuwa taarifa za utafiti huo zipo katika hatua za mwisho kukamilika na baada ya kukamilika watazipeleka  kwa Jeshi la Polisi Mkoani huo kwa ajiri ya hatua zaidi za utekelezaji ili kuzuia vitendo vya rushwa barabarani.


"Sisi kama Takukuru wakati mwingine tunafanya uchunguzi,yaani nikama utafiti kutaka kuangalia tatizo lina ukubwa gani na hatua za kuchukua."amesema Myava

Nakuongeza "Katika kipindi cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka na kabla tulifanya utafiti mdogo wa kuhakikisha tunapata taarifa za usalama barabarani namna zilivo,na sasa tupo katika utaratibu wa kuzikamilisha ili tuwapelekee wenzetu wa Polisi waweze kuona mapungufu yako wapi na ni nani wanaojihusisha na vitendo vya rushwa barabarani.!"

Aidha Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani amesema kuwa siku zote rushwa haipambanwi na mtu mmoja, inatakiwa uwepo  ushirikiano wa Taasisi mbalimbali,hatua hiyo ndiyo inayoweza kufanikisha  mapambano dhidi ya rushwa.

"Taarifa hii itatusaidia sisi na Jeshi la Polisi kufanikisha kudhibiti vitendo vya rushwa vinavyolalamikiwa sana na wananchi hasa wanaotumia vyombo vya usafiri ingawa tunafahamu kwamba Rushwa ni siri kati ya mtu na mtu, inawezekana wakati mwingine wenye vyombo wenyewe ndio wanashawishi".amesema

Ameongeza kwamba "Pia watu wetu baadhi ambao si waadilifu  nao wanakuwa vishawishi katika vitendo vya rushwa hivyo vitendo vya rushwa vipo na sio kwamba havipo kwa sababu ni vitu ambavyo vinalalamikiwa na jamii kila kukicha hususani wale wanaotumia usafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

"Mfano juzi kuna askari wa usalama barabarani ambao wameonekana kupitia picha mtandaoni wakionekana  wakipokea rushwa,tayari hatua zimechukuliwa dhidi yao.

Amesema kuwa hapo awali kulikua na ushirikiano wa Polisi, TAKUKURU na Wadau uliojulikana kama UTATU,lengo la ushirikiano huo  ilikuwa ni kuhakikisha kwamba vitendo vya rushwa barabarani vinatoweka.

"Pia kulikuwa na App iliyokuwa inatumika  kurekodi vitendo vya rushwa vikiwa vinaendelea na baadae unatuma bila kujulikana kwenda kwenye taasisi husika na taarifa kuchakatwa na hatua zinachukuliwa ingawa kwa sasa imelegalega, lakini kama Takukuru tunawajibu kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa."amesema.

Hakuna maoni