Zinazobamba

DKT. BITEKO AKAGUA UJENZI OFISI YA WAZIRI MKUU, NISHATI MJI WA SERIKALI-MTUMBA*

Na Mwandishi Wetu

Dodoma.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amefanya ziara katika Mji wa Serikali, Mtumba na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu pamoja na Wizara ya Nishati ambapo ujenzi wa majengo hayo umekamilika kwa asilimia 88.

Akizungumza mara baada ya kukagua na kupata maelezo ya wataalam na wasimamizi wa majengo hayo, Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko amewapongeza wakandarasi kwa hatua iliyofikiwa na kuagiza majengo yakamilishwe kabla ya mwezi Aprili, 2025.Aidha, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko ametoa maelekezo kwa mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa NHC kuharakisha kukamilisha  Jengo la Wizara ya Nishati ili lianze kutumika kabla ya mwezi Aprili, mwaka huu.

“Serikali chini ya Rais Samia imefanya kazi kubwa, tayari imetoa zaidi ya asilimia 90 ya malipo kwa wakandarasi kwa maana ya kwamba ni kiasi kikubwa zaidi ya ukamilifu wa jengo, najua SUMA JKT mkifanya kwa operesheni mnaweza kukamilisha ujenzi wa jengo hili hata kabla ya muda uliopangwa” amesema Dkt. Biteko

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy Nderiananga amemshukuru Naibu Waziri Mkuu kwa maelekezo yake na kusema Ofisi itaendelea kusimamia kwa karibu ili kuhakikisha malengo yanafikiwa kama ilivyopangwa.

“Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Mhe. William Lukuvi namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa ziara hii ambayo ni chagizo kwetu kuhakikisha kwamba ujenzi wa majengo haya unakamilika kwa wakati kama walivyoomba wakandarasi, kwa kuwa sisi ni waratibu inabidi tuwe mfano kwa wengine” amesema Mhe. Ummy.Naye Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felichesmi Mramba amehakikishia Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuwa,  fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Wizara hiyo ziko katika hatua nzuri na amekuwa akiwasiliana na HAZINA kwa ajili ya upatikanaji wake.

“Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, tuko katika hatua nzuri hata leo asubuhi nimezungumza na PST  (Katibu Mkuu Wizara ya Fedha) na mimehakikishwa kwamba fedha hizo zitapatikana,” amesema Katibu Mkuu Mramba.


Hakuna maoni