ACT WAZALENDO HAITAMBUI MATOKEO YA WAZIRI MCHENGERWA
NA MWANDISHI WETU
Chama cha ACT Wazalendo kimesema hakikubaliani na matokeo yaliyotangazwa na Waziri wa TAMISEMI Mohamed Mchengerwa ambayo yamekipa ushindi wa kishindo Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Matamshi hayo yametolewa leo Novemba 29,2024 na Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa ya Kamati ya Uongozi Taifa ya Chama kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji 2024.
Kwamba mchakato mzima wa uchaguzi umevurungwa kwa kiwango ambacho kimepora madaraka ya wananchi kuchagua viongozi wao.
"ACT Wazalendo tunataka uchafuzi huu wote ubatilishwe na uchaguzi mpya wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji ufanyike baada ya kupata sheria mpya ya uchaguzi huo na Tume Huru ya Uchaguzi," amesema Semu.
Amesema watafanya mawasiliano na Vyama makini vya Siasa na Asasi muhimu za Kiraia ili kuitisha kikao kwa ajili ya kupata mkabala wa pamoja katika kupata ufumbuzi dhidi ya mifumo ya usimamizi na uendeshaji wa chaguzi na vipi kuihami demokrasia hapa nchini.
Semu ametaja Maeneo wanayotaka yafanyiwe kazi kwa pamoja na vyama na asasi makini ni
Mabadiliko ya Katiba ili kupata Katiba Mpya, Sheria za Uchaguzi na uundwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na Sekretarieti Huru ya Tume wakiwemo Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi na Makarani wa Uchaguzi.
Kwamba yote haya yakamilike kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Amesema watakusanya taarifa ya matukio yote ya uchafuzi na uhuni uliofanyika na watatayarisha taarifa kamili ya Chama kuhusu hicho kilichoitwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
Aidha, amesema Chama kinasimamia wanachama na viongozi wote waliokamatwa kuweza kutolewa na inapobidi kuwapatia wanasheria.
Kwamba zaidi ya wanachama wao 60 walikutwa na kadhia ya kukamatwa na kushikiliwa na Jeshi la Polisi wakipambana kudhibiti uhuni uliofanyika kwenye hicho kinachoitwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
Katika hatua ya sasa, amewataka wanachama wao ķutotoa ushirikiano kwa viongozi wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji kutoka Chama cha Mapinduzì (CCM) ambao wametangazwa kuwa washindi bila uhalali hadi hapo uchaguzi huu utakapoitisha na kufanyika upya kwa kuzingatia misingi ya demokrasia ya uchaguzi huru, wa haki na unaokubalika.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni