Zinazobamba

RC MWASA AWATAKA WAKULIMA KAGERA KUZINGATIA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA

KAGERA                             

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa, amewataka wakulima mkoani humo kuzingatia matumizi sahihi ya Mbolea ili kuongeza mavuno na kujiimarisha kiuchumi.

Akizungumza wakati wa kampeni wa Kilimo ni Mbolea wilayani Misenyi Mwassa alisema bei ya Kahawa imeongezeka, lakini bila kuzingatia matumzi sahihi ya Mbolea mavuno yatakua kidogo na uimara wa bei hiyo sokoni hauwezi kumnufaisha mkulima.

Alisisitiza kuwa matumizi sahihi ya mbolea kwenye mazao yanamsaidia mkulima kupata uhakika wa mavuno yake na hivyo kuwa na uhakika wa soko kutokana na mavuno yenye ubora atakayovuna.

“ Unapotumia mbolea kwa usahihi unaoata uhakika wa mavuno yenye ubora yanatakayo kupa bei nzuri sokoni na hivyo kujiongezea kipato chako binafsi na pato la taifa kwa ujumla wake”,alisema Mwassa.

Hata hivyo RC Mwassa alibainisha kuwa Serikali imetatua changamoto ya makali ya bei ya mbolea kwa kuleta mpango wa mbolea ya ruzuku unaosimamiwa na TFRA ili kila mkulima asajiliwe na kunufaika na mpango huo.

“Ndugu zangu wakulima niwakumbushe kuwa Serikali yetu imetatua changamoto ya bei ya mbolea kwa kuleta mpango wa mbolea ya ruzuku unaotekelezwa nchi nzima na ni haki ya kila mkulima kujisajili na kunufaika na bei himilivu ya ruzuku hatimaye kuitumia mbolea hiyo kwa usahihi na kuongeza mavuno”,alibainisha RC huyo.

Aidha aliwataka wakulima kuacha kilimo cha mazoea na kutumia teknolojia mpya kama vile mbolea sahihi ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi. 

Pamoja na hilo RC Mwassa alizindua shindano la usajili wa wakulima kwenye mfumo wa ruzuku ya mbolea na kuhimiza maafisa ugani kutumia vifaa vya kupima udongo ili kuboresha kilimo.

Mamlaka imejikita katika kuhamasisha matumizi ya mbolea kwenye zao la migomba na kahawa ili kuongeza uzalishaji katika mkoa huo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania TFRA Dkt. Anthony Diallo, alisema mamlaka inahimiza matumizi sahihi ya mbolea kupitia majukwaa mbalimbali hivyo ni jukumu la kila mkulima kuitumia elimu wanayopewa na kuketa mabadiliko katika kilimo chao.

Dkt. Diallo aliongeza kuwa wakulima wa Kagera wanalima mazao mbalimbali ya chakula na biashara lakini hawatumii mbolea ipasavyo hivyo kujipunguzia kiasi cha mavuno ambayo wangstahili kuvuna iwapo wangetumia mbolea kwa usahihi.

TFRA kwa kushirikiana na kampuni binafsi ya Black Codes Creativity BCC inaendesha kampeni Kilimo ni Mbolea  inayohamasisha matumizi sahihi ya mbolea na kutoa elimu kwa wakulima, ikilenga kuongeza tija, ambapo kampeni hiyo ya miezi mitatu inahusisha mikoa 10 yenye matumizi kidogo ya Mbolea ikiwemo mkoa wa Kagera na itafikia tamati siku ya mbolea duniani Oktoba 13 mwaka huu.




Hakuna maoni