Zinazobamba

FANYENI KAZI KWA BIDII MTIMIZE NDOTO ZENU: ZUNGU


Na Mussa Augustine.

Naibu spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mussa Zungu amewataka wahititimu wa Chuo Cha Ufundi Stadi Furahika kilichopo Buguruni Malapa Jijini Dar es salaam kufanya kazi kwa bidii na kujiendeleza kitaaluma ili waweze kufikia ndoto zao.a

Naibu Spika Zungu ambaye alikua mgeni rasmi kwenye  mahafali ya 19 ya chuo hicho amesema kwamba serikali imekua ikiweka mazingira rafiki kwa kushirikiana na shule na vyuo binafsi ili kuhakikisha Vijana wa kitanzania wanapata Elimu itakayowasaidia katika Maisha yao na Taifa kwa ujumla.

"Niwapongeze kwa kuhitimu mafunzo yenu katika kada mbalimbali,jambo ambalo ni muhimu zaidi na msiishie hapo mlipoishia na badala yake mjiendeleze zaidi kitaaluma katika ushindani wa soko la ajira"amesema Zungu.

Aidha  amesema ajira zipo za kutosha endapo wahitimu watajituma na kuwa wabunifu zaidi katika kukuza taaluma zao kwa kupitia ubunifu kwani unahitajika zaidi katika ulimwengu wa sasa.

"Serikali imeweka mazingira wezeshi ambayo kipaumbele chake ni vijana,hivyo ni wajibu wenu kujituma na kufanya kazi kwa bidii popote mtakapo ajiriwa au kujiajiri"amesema

Naibu Spika hiyo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewaasa wahitimu hao kuwa na nidhamu huko waendako kwani watakuwa mabalozi wazuri wa Chuo hicho,nakwamba hali hiyo itawasaidia kufanya kazi vizuri nakwa mafanikio makubwa.

Aidha ameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuunga mkono jitihada za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika suala la elimu, kwa kutoa elimu ya fundi kwa vijana bila malipo na kuahidi kusaidia baadhi ya changamoto zinazokikabili Chuo hicho ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chuo Cha Furahika,Dkt David Msuya ameiomba serikali kusaidia kuchangia vifaa vya kuendeshea Chuo hicho kwani wanatoa elimu bila malipo huku mwanafunzi akichangia shilingi elfu hamsini pekee kwa ajili ya mitihani.

"Tukushukuru sana Naibu Spika na nikuombe utuchangie kompyuta pamoja na viongozi wenzako ikiwemo vyerehani na vifaa vingine kwa ajili ya kufundishia kwa vitendo hivyo kwa msaada huo mtakuwa mmewasaidia wanafunzi wa chuo chetu"amesema 

Dkt Msuya amefafanua kuwa jumla ya wahitimu 45 wamehitimu mafunzo ya stadi za kazi (Ufundi)katika fani mbalimbali na wengi waliohitimu katika Chuo hicho wameajiriwa katika sekta mbalimbali hapa nchini.

Ameongeza Kuwa wameamua kutoa elimu ya Ufundi kwa vijana wa kike na kiume ili kusaidia kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya na biashara ya kuuza miili kwa vijana wa watoto wa kike ambayo husababishwa na vijana hao kukosa elimu ambayo huwasaidia kupata ajira au kujiajiri.

Hakuna maoni