Zinazobamba

FCS NA TCRA CCC KUSHIRIKIANA KULINDA HAKI ZA WATUMIAJI WA MAWASILIANO.

Na Mussa Augustine 

Asasi ya Kiraia ya Foundation For Civil Society (FCS) na Baraza la Ushauri la watumiaji wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA CCC) zimetiliana saini ya makubaliano ya miaka mitatu yenye lengo la kuimarisha juhudi za kulinda haki za watumiaji wa huduma katika sekta ya Mawasiliano Nchini Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Agost 6 ,2024 jijini Dar es salaam Mkurugenzi Mtendaji wa FCS  Bw.Justice Rutenge amesema kwamba Ushirikiano  huo unatambua umuhimu wa kuwalinda watumiaji dhidi ya mbinu za kibiashara zisizo za haki katika soko.

" Ubia huu unalengo la kuhakikisha haki na uwajibikaji katika kutoa huduma kwa watumiaji na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi wanaponunua na kutumia bidhaa na huduma za kulinda haki za watumiaji (Consumer Protection)hivyo unachangia maendeleo ya masoko na ukuaji wa biashara" amesema Rutenge.

Nakuongeza kuwa" Biashara zinazoheshimu sera za kulinda watumiaji na kuwapa wateja wao kipaumbele hujijengea hadhi na kuziweka katika nafasi nzuri kiushindani,hii huzihakikishia biashara hizo uwepo wa wateja wa uhakika na kuweka meingi mzuri wa ukuaji.

Aidha ameendelea kufafanua kuwa katika soko la sasa lenye mabadiliko ya haraka,uadilifu katika biashara unategemea kwa kiasi kikubwa kulinda haki za watumiaji dhidi ya mbinu zisizo za haki na udanganyifu katika biashara.

Bw.Rutenge amesema kwamba Wafanyabiashara Wana nafasi muhimu katika kuhakikisha uwazi na usahihi katika shughuli zao,hivyo FCS na TCRA CCC zimeunganisha nguvu katika kubuni na kutekeleza mradi unaolenga kulinda haki za watumiaji wa bidhaa na huduma za Mawasiliano Nchini Tanzania.

Aidha amesisitiza umuhimu wa asasi za kiraia kushiriki katika kuimarisha mifumo ya kulinda na kutetea haki za watumiaji wa uhuduma na bidhaa,nakudai kuwa kwa miaka mingi FCS imekua ikisisitiza maendeleo yaliyojikita katika kuwanufaisha wananchi zaidi.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TCRA CCC ,Bi.Mary Shao Msuya amesema kwamba Baraza hilo limeanzishwa kwa lengo la Kuhakikisha maslahi ya watumiaji wa huduma za Mawasiliano za TEHAMa,huduma za Utangazaji,huduma za Posta,Vifurushi na Vipeto.

Amesema kuwa huduma za Mawasiliano nchini zinaongezeka kutokana na ukuaji wa kasi wa teknolojia ambapo kwa mujibu wa takwimu za TCRA ,kufikia Mwezi June 2024 kuna kadi za simu milioni 76.6,watumiaji wa internet milioni 39.3,akaunti za pesa mtandao milioni 55.7, ambapo idadi hiyo itaendelea kuongezeka na huduma mpya zitaongezeka kutokana na kukua kwa Teknolojia ya kidijitali.

"Ukuaji huu wa teknolojia ni muhimu hasa wakati nchi yetu imejikita kwenye uchumi wa kidigitali ,Mawasiliano yanaweza kufikisha taarifa kwa wakati ,uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo Biashara,uzalishaji ,Elimu,Afya na upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha.

Hakuna maoni