Zinazobamba

KILIMO NI MUHIMILI WA UCHUMI WA TANZANIA

Na Mwandishi wetu, Nzega Tabora 

Sekta ya Kilimo inatajwa kuwa muhimili wa uchumi wa Tanzania, ikiajiri takribani theluthi mbili ya nguvu kazi ya taifa na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda, asilimia 100 ya usalama wa chakula, na zaidi ya asilimia 26 ya pato la taifa.

Akizungumza katika mkutano na wakulima katika kijiji cha Ndala Wilayani Nzega Mkoa wa Tabora, Mkuu wa Wilaya hiyo Naitapwaki Tukai alisema, maendeleo ya mwananchi na taifa yanategemea ufanisi katika sekta ya kilimo hivyo ni wajibu wa kila mkulima kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea.

Mh. Tukai alibainisha kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka bilioni 294 mwaka 2021/22 hadi trilioni 1.24 mwaka wa fedha wa 2024/25 ambapo lengo hasa ni kufanya mapinduzi katika Sekta ya Kilimo kwa kuongeza tija.

"Nawaomba kwa pamoja tuunge mkono jitihada za serikali za kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inaendelea kuimarika, lakini pia tumuunge mkono Mh. Rais kwa kujitokeza kwa wingi kusajiliwa kwenye daftari la wakulima na hatimaye tunufaike na mbolea za ruzuku ili mabadiliko yanayofanywa katika sekta ya kilimo yaendelee kutunufaisha wakulima na taifa kwa ujumla", alisisitiza Naitapwaki

Aidha aliongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa mbolea kwa bei ya ruzuku kwa misimu mitatu mfululizo,  kuhakikisha mkulima anapata mbolea kwa bei himilivu na kuwakumbusha wakulima kuitumia mbolea hiyo kwa usahihi ili ilete matokeo mazuri wakati wa mavuno. 

"Tukipata matokeo mazuri wakati wa mavuno tutakua na uhakika wa chakula kwa mkulima mmoja mmoja, uhakika wa chakula kwa Taifa letu lakini pia tutapata ziada kwaajili ya biashara ili kukidhi mahitaji mengine ya familia", aliongeza.

Nae mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Anthony Diallo alitumia wasaa huo kuwakumbusha wakulima kutumia mbolea sahihi, kwa wakati sahihi, kwa kipimo sahihi na eneo sahihi la mmea.

"Ndugu zangu wakulima leo tumekusanyika hapa ili tukumbushane kupitia kampeni yetu ya Kilimo Ni Mbolea tuone mabadiliko katika mavuno yetu kwa kuzingatia kanuni nne muhimu za matumizi sahihi ya mbolea ili tuendelee kupata mavuno mengi na bora",alisema Dkt. Diallo.

Pamoja na hilo Dkt. Diallo aliwakumbusha wakulima kusajiliwa kwenye daftari la wakulima na kuingia kwenye mfumo wa kidigitali wa mbolea ya ruzuku ikiwa ni moja kati ya hatua muhimu kwa uzalishaji tija na ukuaji wa sekta ya Kilimo nchini.

"Kwasababu Kilimo ni Mbolea hatuna budi kuchangamkia fursa ya usajili tukiwa na kitambulisho cha NIDA au cha mpiga kura baada ya hapo tutumie mbolea kwa kuzingatia kanuni nne muhimu za mbolea ambazo ni nunua mbolea sahihi, tumia mbolea kwa wakati sahihi, kwa kipimo sahihi na sehemu sahihi, kwa kuzingatia hayo tutaendelea kuneemeka kwa chakula na kipato pia", alibainisha Dkt. Diallo.

Vilevile Dkt. Diallo aliongeza kuwa kwa kusajiliwa na kuoata mbolea ya ruzuku wakulima watakua wameifanikisha azma ya Serikali, ya kukifanya Kilimo kiwe biashara na sio adhabu.Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Joel Laurent alisema kuwa TFRA inafanya kampeni ya Kilimo ni mbolea katika maeneo tofauti nchini ili kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na kuhamasisha wakulima kujisajili kwenye daftari la wakulima ili wanufaike na mbolea za ruzuku.

Aliongeza kuwa lengo la usajili wa wakulima ni kupata takwimu sahihi za wakulima nchini zitakazosaidia serikali kuweka mipango sahihi ya kuwahudumia wakulima kwa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea, mbegu na mahitaji mengine.

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inaendelea kutumia majukwaa mbalimbali ikiwemo kampeni yake ya Kilimo ni Mbolea kuelimisha wakulima matumizi sahihi ya mbolea na kuwakumbusha wakulima kujisajili ili kunufaika na fursa ya mbolea kwa bei ya ruzuku.

Hakuna maoni