Zinazobamba

HALMASHAURI YA KIGOMA YAPATIWA MAFUNZO JINSI YA KUKABILIANA NA MAAFA

 

Na Mwandishi Wetu,

KIGOMA

Serikali inasimamia na kuratibu shughuli za kuzuia na kukabiliana na majanga kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2004 na Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na 6 ya Mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022 kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa inayotekeleza majukumu yake chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo suala la kuzuia na kukabiliana na majanga ni mtambuka na linahitaji nguvu za pamoja katika kulishughulikia.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya kujenga uelewa juu ya upunguzaji wa madhara ya maafa katika jamii iliyofanyika tarehe 26 agosti, 2024 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Mkurugenzi Msaidizi  Idara ya Menejimenti ya Maafa sehemu ya Afya Moja  Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Salum Manyatta amesema, kuongezeka kwa matukio ya majanga ambayo yamekuwa yakisababisha maafa na kuathiri mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii, Maafa haya yamekuwa yakisababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo, ulemavu wa kudumu, upotevu na uharibifu wa mali, miundombinu na mazingira.

Hivyo Dkt. Manyatta amewataka viongozi wa serikali za vijiji kuhakikisha inafahamu namna ya muundo wa maafa unavyofanya kazi ili kurahisisha uapatikanaji wa taarifa kwa ajili ya kupata namna ya kujiandaa kukabiliana  kabla maafa hayajatokea

“Tunasema serikali Kijiji ni serikali inayotambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini kwenye ngazi ya Kata tunajulikana kama kamati ya maendeleo ya kata kwa hiyo sisi tunakaa nao kama kuna maeneo yanahusisha Kata ujenzi wa kituo cha Afya, ujenzi wa Zahanati, ujenzi wa Kituo cha Polisi tunafanya kwa kile ambacho tunakiona kinatukwamisha kwenye kazi hivyo tumekuja hapa kwa masaa machache kuna mada mtajifunza kwa ajili ya uelewa wa pamoja  maana utekelezaji wa masuala ya maafa yapo kwenye maeneo yetu, maafa hutokea kwa watu na watu wapo kwetu hivyo tukipata uelewa huu tutaweza kukabili jambo hili” alisema Dkt. Manyatta

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bw. Bruno Francis amezitaka Kamati za Maafa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kutumia  mafunzo yanayotolewa ya  jinsi ya kukabiliana na Maafa ili kupunguza athari na uharibifu wa mazingira katika maeneo yao.

“Sasa leo tumepata fursa ambayo ndio haya mafunzo hivyo kila mtu awe makini tusikilize ili lolote litakalotokea na hatuombei maafa yatokee kwa sababu hakuna mtu anayaleta maafa, yanajitokeza tu bila kutarajia kwa hiyo tutakapojifunza hapa na tukienda kupeana maagizo kuwa kila mmoja atekeleze wajibu wake katika ngazi zote” alisema Bw. Bruno

Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa  (IOM) imefanya semina ya kujenga uelewa juu ya upunguzaji wa madhara ya maafa katika jamii ambapo semina hii itaendeshwa kwa siku mbili kuanzia Agosti 26 hadi Agosti 27, 2024 katika Halmashauri ya wilaya ya Kigoma.



Hakuna maoni