Zinazobamba

Zoezi la uhamaji Ngorongoro: Dkt Samia apongezwa... wananchi 515 kutoka kaya 72 nao wahama kwa hiari




Na Suleiman Magali

Wananchi waliohamia kwa hiari katika Kijiji cha Msomera Mkoani Tanga wamempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi ikiwamo kuandaa huduma bora za kijamii Kijiji cha Msomera.

Mmoja wa wahamiaji hao, Bw. Mingati Molel akizungumza na waandishi wa habari kijini Msomera, mambo walioahidiwa na serikali ni uwepo wa huduma bora za kijamii, ahadi hiyo imetekelezwa kwa vitendo hasa baada ya kukamilika kwa shule na kituo cha afya.

Kwa kweli tunamshukuru sana Rais Samia kwa kutekeleza ahadi zake, wengi wetu tulikuwa na hofu juu ya eneo hili, lakini tumejionea ni eneo salama na linafaida nyingi.

Amesema mbali na uwepo wa huduma za kijamii, pia eneo la Msomera linamazingira mazuri ya kulima na kwamba yeye amelima na kufanikiwa kupata mavuno ya kuridhisha.

“Kama mnavyoona, hili ni shamba langu, mahindi yamestawi hivi, pia toka nifike hapa nimefanya uwekezaji, nimeweka mashine ya kusaga ambapo mke wangu ndiye anayefanya kazi, kwa kweli Msomera ni pazuri” amesema Molel

Huku tunaruhusiwa kutembea muda wowote, kufanya shuguli za uzalishaji, pia kuendeleza mashamba yetu. Kule ilikuwa ni kama tupo kifungoni, ilikuwa ikifika saa 12 wote tunatakiwa kuwa tayari tumewasili nyumbani, vinginevyo hutaruhusiwa kuingia

Vilevile kule ilikuwa ni ngumu kufanya shughuli za maendeleo, ilikuwa ni kufuga na kulala tu,” aliongeza

Kwanza tunairaumu serikali kwa kutufanya tusifanye kazi kwa miaka yote 60, mapaka umri huu ninamiaka 60 lakini sijafanya shughuli ya maendeleo, huku ni kupoteza muda na nguvu kazi bure, tulitakiwa tufike huku mapema ili tufanye maendeleo,” aliongeza

Mwingine ni Petro Tengesi ambaye ameungana na Molel kumshukuru Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwa wananchi wa Ngorongoro.

Tengesi amesema anamshukuru kwa kuendelea kuwajengea mazingira bora nje ya hifadhi ikiwemo ulipwaji wa stahiki zao za kuhama, kusafirishiwa mizigo yao pamoja na kuboreshewa huduma za kijamii nje ya hifadhi.

Mwitikio wa kuhama waongezeka…

Idadi ya wananchi wa Ngorongoro wanaohamia Msomera na maeneo mengine imezidi kuongezeka ambapo kundi kubwa lenye kaya 72 wananchi 515 na mifugo 2,206 limeagwa Januari 18, 2024 baada ya kujiandikisha na kuamua kuhama kwa hiyari.

 

Wananchi hao 515 wamehamia Kijiji cha Msomera handeni Mkoani Tanga kwa hiari.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo, meneja wa mradi wa kuhamisha wananchi waishio ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Fedes Mdala ameeleza kuwa mpaka Januari 18, 2024 jumla ya kaya 749 zenye watu 4,337 na mifugo 19,915 zimehama ndani ya hifadhi.

Watu hao wamehamia maeneo yaliyopangwa na serikali pamoja na maeneo mengine ambayo wamechagua wenyewe.



Naye, Kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro Richard Kiiza ameeleza kuwa kundi ambalo limeondoka Januari 18, 2024 ndilo kundi kubwa kuwahi kutokea toka kuanza zoezi la kuhamisha na kwamba hayo ni mafanikio makubwa yanayoonesha kuwa elimu imeanza kueleweka

“Hili ndilo kundi kubwa tangu kuanza utekelezaji wa zoezi hili tunaamini kadri ujenzi wa Nyumba za makazi unavyoendelea Kijiji cha Msomera, kitwai na Saunyi idadi ya wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiari itaendelea kuongezeka.

Aidha mesema takwimu zinaonyesha mpaka januari 18, 2024  zaidi ya kaya 1,070 zimeshajiandikisha kuhama na zoezi la uhamasishaji na uelimishaji linaendelea.


vilevile, zoezi la ujenzi wa Nyumba 5,000 katika Kijiji cha Msomera, Saunyi na Kitwai linaendeela chini ya SUMA JKT na tayari zaidi ya nyumba 360 zimeshakamilika na nyumba zingine zaidi ya 2,000 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi.


Kiiza amewataka wananchi waliohama kwa hiari kuendelea kuwa mabalozi wa kuwahimiza wananchi waliobaki kujiandikisha kuhama kwa hiari ili wanufaike na Maisha bora yaliyoandaliwa na Serikali nje ya Hifadhi.


Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo ameeleza kuwa wananchi wanaohama kwa hiyari wanapewa stahiki zao zote za msingi ikiwepo nyumba yenye hati kwenye eneo la ukubwa wa ekari 2.5, shamba la kulima la ekari tano, huduma za maji, shule, afya, barabara, mabwawa, majosho, minada, umeme na huduma za mawasiliano na kupata uhuru wa kufanya shughuli za kilimo na kuishi Maisha huru tofauti na hifadhini.


Kanali Sakulo ameelekeza uongozi wa NCAA kuendelea kutoa elimu, uhamasishaji na uandikishaji kwa wananchi walio tayari kuhama kwa hiari na kuhakikisha kuwa kila mwananchi aliyejiandikisha kuhama anahamishwa kwa wakati, kupata stahiki zake zote na kuhakikisha wananchi wanaohama hawarudi tena maeneo ambayo wameshahama kwa kuwa Serikali yetu imeshawajengea mazingira wezeshi yenye huduma zote muhimu za kijamii.

 


Hakuna maoni