Zinazobamba

DTK GWAJIMA AVITAKA VITUO VYA KULELEA WATOTO MCHANA VIZINGATIE MAADILI NA DESTURI ZA KITANZANIA.

Na Mussa Augustine.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wanawake na Wenye Mahitaji Maalum Dkt Dorothy Gwajima amewataka wamiliki wa Vituo vya kulelea watoto wadogo Mchana  (Day care ) kuzingatia Maadili na Desturi za kitanzania nakwamba  watakaobainika wanafanya  kinyume agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungiwa vituo vyao.

 Pia Waziri huyo amewataka wamiliki wa vituo vya watoto wadogo Mchana na shule za awali kujisajili ili waweze kupewa miongozo ya kuendesha vituo hivyo kwa mujibu wa sheria.

 Dkt Gwajima ametoa kauli hiyo Jijini Dar es salaam Desemba 13,2023  wakati akifungua Mkutano wa Umoja wa  wamiliki wa vituo vya Kulelea Watoto Wadogo Mchana (Day care) Dar es salaam( UVIWADA )ikiwa ni mwendelezo wa   Maadhimisho ya miaka 50 ya chuo cha ustawi wa jamii.

 Aidha amesema kwamba Serikali kupitia Wizara hiyo haitawavumilia wamiliki wa Vituo vya kulelea Watoto Mchana  watakaobainika kwenda kinyume na Maadili na Desturi za kitanzania.

 Amesema wamiliki wa Vituo vya Kulelea Watoto Mchana wanapaswa kutambua na kuzingatia sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali iliyowekwa na Serikali katika uendelezaji wa vituo hivyo.

 "Mmiliki yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maadili na desturi za kitanzania nitafika nae mbali kisheria, hivyo nawasihi sana UVIWADA muungane wenyewe, mshauriane wenyewe, mtiane moyo wenyewe ili muweze kuwabaini wanaokwenda kinyume na maadili ya kitanzania"amesisitiza  Dkt Gwajima 

 Aidha ameupongeza UVIWADA kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya katika jamii kwani wamekuwa wakiwafanya  watoto wa Taifa hili kuwa na maadili mema pamoja na kuwakinga na vitendo vya ukatili.

 Pia Dkt Gwajima ambaye amekua mlezi wa  UVIWADA ameahidi kuwa nao bega kwa bega katika kuhakikisha malezi ya watoto yanatolewa kwa misingi bora nakuweza kuwa na ustawi mzuri wa watoto.

 katibu wa UVIWADA   Josephine Rutashobya 

Awali katibu wa  UVIWADA Mkoa wa Dar es salaam  Josephine Rutashobya akiwasilisha risala  ya Umoja huo aliiomba  Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Makundi Maalumu kuangalia kwa mapana zaidi masharti ya usajili wa vituo vyao kulingana na mazingira halisi hususani Jijini Dar es salaam.

 Aidha  umoja huo pia uliiomba na kuishauri Serikali kutovifungia  vituo ambavyo bado havijapata usajili na badala yake  viongezewe muda walau hadi mwezi June 2024 ili  viendelee na mchakato wa usajili.

 Pia  wameiomba Serikali kuruhusu vituo hivyo viruhusiwe kuwa na watoto hadi miaka sita,na mwongozo wake uboreshwe kwa madai kuwa shule za awali ni chache,nakwamba shule za Serikali zisichukue watoto wa chini ya miaka mitano maana huko hakuna uchangamfu wa awali wa watoto.

 Maombi mengine ni pamoja na vituo vya kulelea watoto Wadogo Mchana kua vinatoa huduma tu kwenye jamii hivyo Serikali ivipunguzie mzigo wa Kodi.

 Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVIWADA  Shukuru Mwakasege amesema  kuwa asilimia kubwa ya  Wamiliki wa vituo vya kulelea watoto mchana hawajasajiliwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo masharti magumu nakuiomba serikali kupunguza masharti hayo.

 Hata hivyo Mwakasege amesema  wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha maelekezo yote yaliyotolewa wanayafanyia kazi.

 

 

Hakuna maoni