Zinazobamba

Waziri Ummy Asema Mpaka Sasa Hakuna Mgonjwa wa Homa ya Mgunda,Adai Lindi ipo Salama.

Na Mussa Augustine.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema  kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa wa homa ya Mgunda (LEPTOS) aliyelazwa katika kituo chochote cha afya, nakwamba wagonjwa wote wamesharuhusiwa kurudi nyumbani na wanaendelea na shughuli zao .
Hayo ameyasema leo jijini  Dar es salaam Waziri wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa Ugonjwa huo ambao ulizuka hivi karibuni Mkoani Lindi na kusababisha watu ishirini kuthibitishwa kuugua ugonjwa huo huku watu watatu kati yao kufariki dunia.

"Hivi sasa hakuna Mgonjwa aliyelazwa wote wamesharuhusiwa kurudi nyumbani na wanaendelea na shughuli zao ,hii inaendana na sayansi inayojulikana kwa ugonjwa huu kuwa unatibika Kwa kutumia dawa ambazo zinapatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini." Amesema.

Aidha Waziri Ummy  amendelea kusema kuwa maandiko ya kisayansi yanaeleza kuwa Kwa kawaida ugonjwa huo unakua na dalili ambazo sio kali Kwa asilimia 90 isipokuwa Kwa wagonjwa wachache (asilimia 10) Wanaweza kuwa na dalili Kali ikiwemo kutokwa na damu nakuathirika viungo ikiwemo Figo, na ini.

Amesema  kwamba timu ya ufuatiliaji imebaini kuwa miongoni mwa watu wanaotangamana na wagonjwa hao hakuna alieonesha dalili za ugonjwa huo hadi kufikia sasa,hii inadhihilisha kwamba ni mara chache ugonjwa huu huambukizwa kutoka binadamu mmoja kwenda mwingine.

" Uwezo wa kuchunguza kwa njia ya maabara upo hapa nchini wananchi wanatakiwa kutokuwa na hofu kwani ni Muhimu wanapokuwa na dalili za ugonjwa huu kuwahi kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata matibabu stahiki kwa  wakati" amesema.

Amesisitiza kuwa ugonjwa wa homa ya Mgunda huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda Kwa binadamu kupitia Uchafuzi wa Mazingira ikiwemo vyanzo vya maji vilivyochafuliwa na Wanyama wenye maambukizi  ya ugonjwa huo.

Amebainisha  kuwa maambukizi hayo hutokana nakugusa mkojo au majimaji mengine ya Mwili kutoka kwa wenye mabukizi,kugusa udongo au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa  Wanyama wenye maambukizi,kunywa maji yaliyochafuliwa ma navimelea vya bakteria wa ugonjwa huo.

"Bakteria wanaweza kuingia mwilini kupitia ngozi,utando wa macho,pua,mdomo,nakupitia ngozi ngozi yenye mikwaruzo kwani maambukizi ya ugonjwa huu kutoka kwa binadamu mmoja kwenda Kwa mwingine hutokea kwa nadra sana." Amesema

Hata hivyo  Waziri Ummy ametoa wito kwa wagonjwa wenye dalili za ugonjwa huo ikiwemo homa,kuumwa kichwa,maumivu ya misuri,uchovu wa mwili,mwili kuwa na rangi ya manjano,macho kuvilia damu,kutokwa damu puani,kukokoa damu,kichefuchefu na kuharisha wahakikishe wanafika kwenye vituo vya kutolea huduma za matibabu mapema.

Ikumbukwe kuwa taarifa za ugonjwa wa homa ya Mgunda uliozuka hivi karibuni Mkoani Lindi nakusababisha taharuki Kwa wananchi,ilitolewa rasmi julai 18 mwaka huu,baada ya uthibitisho wa kimaabara ambapo hadi sasa hakuna ugonjwa mwingine mpya uliozuka.

Hakuna maoni