Maonesho ya Vyuo Vikuu mnazi mmoja na fursa ya wazazi kufanya maamuzi sahihi
Maonyesho ya vyuo Vikuu Tanzania (TCU) yameanza kwa kasi viwanja vya mnazi mmoja, lengo hasa la maonyesho haya ni kuwezesha wazazi na wanafunzi waliomalima elimu ya sekondari pamoja na vyuo vya astashahada kupata fursa ya kupata taarifa mbalimbali juu ya vyuo wanavyotaka kujiunga navyo katika mwaka wa masomo 2022/2023 Mwaka huu maonyesho haya yamealika baadhi ya vyuo kutoka nchi mbalimbali duniani pamoja na zile za ukanda wa Afrika Mashariki kama Kenya na Uganda na taasisi zinazohusika na kuwatafutia wanafunzi vyuo nje ya Tanzania. Hakika maonesho haya yanatoa fursa kwa wazazi/walezi kufahamu kwa kina taarifa muhimu za vyuo husika. Jana mwandishi wetu alipata bahati ya kutembelea mabanda mbalimbali viwanjani hapo kufahamu kwa kina mambo mbalimbali yanayoendelea vyuoni Banda la RUCU, Iringa Katika banda la chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU), yapo mengi ya kujionea, chuo kimesheheni haswa wataalam ambao wanafafanua shughuli zinazofanywa na Taasisi yao. Ni wazi kuwa mzazi/mlezi akifika Mnazi mmoja na kuwatembelea bila shaka atapata elimu nzuri kuhusiana na uchaguzi wa fani ya watoto wao na faida zake.
RUCU, ni chuo ambacho kina mipango mingi ya kutatua changamoto za jamii, kupitia tafiti ambazo wanafanya chuo hicho kimeweza kuja na mitaala ambayo ina majawabu ya changamoto zinazoikabili jamii. Mfano, RUCU imekuja na tafiti/ubunifu wa kukukabiliana na changamoto za kimazingira Kama vile Mbu wanaoambukiza Ugonjwa wa Malaria. Yote haya ni mafunzo yanayotolewa chuoni. Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi wa Kozi za Shahada na zisizo za Shahada wa Chuo hicho, Dkt Wille Migodela, alisema RUCU ni sehemu sahihi ya kulea vipaji vya vijana. Mtaalam huyo alisema mbali na kutoa kozi mbalimbali lakini Elimu ya utafiti wa Ubunifu imekua ikipewa kipaumbele ili kumsaidia mwanafunzi anayehitimu kuondokana na zana ya kutegemea kuajiliwa na badala yake aweze kujiajili mwenyewe. Vilevile alisema kupitia tafiti zinazofanywa na wanafunzi wao, wamefanikiwa kubuni kifaa kinachoweza kutambua uzito wa mzigo unaobebwa kwenye gari, umuhimu wa kifaa hicho ni kupunguza msongamano wa magari kwenye mizani yetu. Watu wamekuwa wakitumia muda mrefu kusubiri kupima, lakini kitendo cha kufunga kifaa hicho cha RUCU dereva halazimiki kuingia tena mizani kwani uzito utakuwa unaonekana kupitia kifaa hciho. "Magari yanatumia muda mrefu kukaa kwenye foleni ya mzani kupima uzito wa mzigo,sisi kama RUCU tumekuja na suluhisho la kubuni kifaa Cha kisayansi kitakachoonyesha ukomo wa uzito wa mzigo unaotakiwa kupakiwa" amesema Dkt Migodela Pia wametengeneza kifaa kinaitwa "Analogy wheel" kazi yake ni kupima umbali kwenye tambarare (horizontal distance) wakati wa kufanya Survey (upembuzi). Kifaa kinafanya kazi mbadala wa Chain (mnyororo) ambao kwa mda mrefu umekuwa ukishindwa kutupa vipimo halisi kwasababu ya masikio(oval shape) yanayo uunganisha na pia chain inatumia mda mrefu kupima urefu ardhini. …Nafasi za masomo chuoni RUCU Aidha akizungumza kuhusu nafasi za masomo chuoni kwao, Mkurugenzi huyo alisema nafasi zipo nyingi na kwamba wamejipanga kuwasaidia wanafunzi wote ambao wanataka kujiunga na chuo chao, hasa wale watakaopata fursa ya kutembelea banda lao.
“Kwa mwaka wa masomo 2022/ 2023 tunatarajia kudahili wanafunzi wapatao 1,400 ambapo wanafunzi wa Cheti na Diploma ni 700 na wengine 700 ni Shahada (Digree),” alisema Chuo cha SUZA chanzisha kozi mpya Katika banda la SUZA, Mkuu wa Kitengo Cha Uhusiano na Masoko wa Cho cha SUZA Khadija Sadiq Mahumba alisema chuo chao kimekuja Mnazi mmoja na fursa nyingi ikiwamo ujio wa kozi ya Kiswahili kwa ngazi ya uzamivu Pia Mtaalam huyo wa mahusiano alisema kozi zinazotolewa na Chuo hicho zimelenga kuwafanya wanafunzi waweze kujiajiri, kwani wanapatiwa mafunzo mazuri ya kujitegemea.
Aidha katika kuunga mkono sekta ya elimu nchini chuo kimeanzisha kozi mpya ya Shahada ya Uzamivu kwenye Sayansi ya Teknolojia ya Habari (IT) katika mwaka wa Masomo 2022/ 2023.
Pia, alisema kwamba chuo hicho kinatarajia kudahili wanafunzi wapatao 2000 Kwa programu mbalimbali zikiwemo za elimu, afya, Kilimo kwa ngazi mbalimbali ikiwemo Astashahada, stashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili na Uzamivu. Kuhusu fursa ya Kiswahili, Hadija alisema chuo kinatarajia kutoa programu ya Shahada ya Uzamivu (Phd) ya Lugha ya Kiswahili, na kuwasihi wanafunzi wanaotaka kujiunga na SUZA wachangamkie fursa ya somo hilo Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Uhusiano na Masoko SUZA alisema kwa wanafunzi watakaosoma kozi za utalii watapata fursa ya kusoma lugha mbalimbali za kigeni ikiwemo lugha ya Kireno, Kichina Kifaransa, Kijerumani, na kwamba chuo hicho pia kinatarajia kuanza kufundisha Programu ya lugha ya Kikorea.
Pia alisema katika dirisha la pili la udahili wanatarajia kudahili wanafunzi kwa program mpya za Shahada ya Uzamili ya Benki na Fedha (MSc Benking & Finance) pamoja na Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Fedha na Biashara ( MBA-Finance).
Katika hatua nyingine, bosi huyo wa kitengo cha mauzo wa SUZA alitoa wito kwa wazazi na walezi kutembelea banda la chuo hcho kupata elimu Zaidi. “Ningependa kuwaomba wazazi wawalete wanafunzi kwenye banda letu hapa Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam wajionee kozi tunazofundisha ili wafanye maamuzi sahihi yakujiunga na chuo chetu chenye fursa ya kupata ajira nje na ndani ya nchi" alisema Khadija. Maonesho ya vyuo vikuu yameanza huku Vyuo Vikuu vya nje vikionekana kuwa kivutio kwa watu wengi. Vyuo hivyo ambavyo viko kwenye mabanda ya Global Education Link (GEL), ni pamoja na MM, Sharda, CT, Geomedi, GELISM, Lovely Professional University, LPU, PDEU. Vingine ni vya kutoka nchi za India, Iran Cyprus, Uturuki, Georgia, Canada, Australia, Urusi, Dubai, Poland, Mauritius, Marekani na Uingereza. Kati ya vyuo hicho, Chuo cha CT cha India kupitia kwa Naibu Mkurugenzi wa chuo hicho, Gaurav Sharma, kimetangaza neema kwenye fani za tiba, na kuwashauri wanafunzi watanzania kuchangamkia fursa. Sharma alisema wametoa punguzo la asilimia 50 kwa wanafunzi watanzania watakaodahiliwa kwenda kusoma kwenye chuo hicho. Alisema kuna Zaidi ya watanzania 100 wanasoma chuoni kwao katika fani za ufamasia, taaluma ya usingizi, teknolojia ya maabara, mionzi, teknolojia ya chumba cha upasuaji, physiotherapy (mamacheza) na Shahada ya Afya ya jamii. Alisema nchi nyingi duniani zinakabiliwa na upungufu wa wataalamu wa usingizi, mionzi na wale wa teknolojia inayotumika kwenye vyumba vya upasuaji na chuo hicho kimekuwa kikitoa wataalamu wengi kutoka mataifa mbalimbali. Alisema chuo cha CT pia kimekuwa kikitoa wataalamu wa fani za akili bandia (artificial intelligence) na teknolojia ya hali ya juu kwa watu wanaofanyiwa matibabu ya moyo. Alisema pia kimekuwa kikizalisha wataalamu wa kuhudumia wagonjwa mahututi na namna ya kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji kuchujwa au kubadilishwa damu (Dialysis).
Wakala wa Elimu Nje ya Nchi, Global Education Link (GEL) imefanikiwa kuleta nchini vyuo 10 ili kushiriki maonesho ya 17 ya vyuo vikuu yanayoendelea katika viwanja vya mnazi mmoja, Dar es Salaam. Miongoni mwa vyuo hivyo ni pamoja na MM, Sharda, CT, Geomedi, GELISM, Lovely Professional University, LPU na PDEU. Mkurugenzi wa GEL, Abdulmalik Mollel, alisema wameamua kufanya hivyo ili kutoa uwanja mpana kwa wazazi kufanya maamuzi sahihi. Alisema kuna faidia kubwa kwa watu kwenda kusoma nje, kwani wanachota ujuzi na kulisaidia taifa. Alisema zamani wazazi waliogopa kuruhusu watoto wao kwenda nje ya nchi kusoma wakidhani kwamba hawatarejea lakini wengi wamekuwa wakichukua ujuzi na kuja kuutumia hapa nyumbani. “Wanafunzi wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu wanapaswa kutembelea mabanda ya Global Education Link kwenye maonyesho ya Mnazi Mmoja kwasababu kuna uwakilishi wa vyuo 10 kutoka nje ambao watawaeleza kuhusu kozi wanazotoa na wataalamu wetu watawapa taarifa ili wawe na chaguo sahihi,” alisema. Ends,
|
Hakuna maoni
Chapisha Maoni