Ni khutuba ya Matumaini, Rais Magufuli akilifungua Bunge la 12, aanika Taswira ya Miaka Mitano ya Serikali Yake
Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli leo amefungua rasmi Bunge la 12 ambapo ametaja baadhi ya vipaumbele ambavyo serikali yake itajikita zaidi katika miaka mitano ijayo.
Baada ya kutoa shukrani kwa Watanzania na mamlaka mbalimbali kwa namna zoezi la uchaguzi lilivyofanyika kwa uhuru, haki na kwa amani amesema kwenye miaka mitano ijayo serikali itafanya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusimamia utawala bora, kusimamia nidhamu kwa watumishi pamoja na kuboresha maslahi yao.
Mambo mengine ambayo amesema serikali yake itaboresha ni shughuli za uvuvi baharini ambapo zitanunuliwa meli nane za uvuvi ambapo nne zitakuwa upande wa Zanzibar na nne upande wa Tanzania Bara ili kuboresha sekta hiyo na kuwanufaisha Watanzania.
Kwa miaka mitano ijayo, serikali imeahidi kuboresha vitambulisho vya wajasiriamali wadogo kwa kuviwekea taarifa muhimu pamoja na picha ili waweze kuvitumia kwenye shughuli nyingine ikiwa ni pamoja na kuombea mikopo kwenye benki.
Aidha, amesema kuwa anategemea ushirikiano kutoka Bunge la 12 lakini amelitahadharisha kuwa lisiwe bunge la kukubali na kupitisha kila kitu badala yake wakosoe pale panapohitaji kukosoa kwa lengo la kujenga na si kukosoa kwa lengo la kukosoa.
Amesema pia serikali yake itaboresha sekta ya habari na sanaa ambapo ametumia wasaa huo kuwapongeza wasanii waliochaguliwa kuwa wabunge pamoja na waandishi wa habari kwa namna wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuuhabarisha umma juu ya yale yote yanayotekelezwa na serikali.
Uboreshaji wa sekta ya viwanda na kilimo na mambo ambayo serikali imepanga kufanya katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kwani sekta hizo ni muhimu katika kufikia uchumi wa viwanda na zinagusa idadi kubwa ya Watanzania.
“Tumepanga kuendeleza jitihada za kukuza uchumi. Tutahakikisha ukuaji wa uchumi unanufaisha wananchi kwa kuinua vipato vyao, kupunguza umasikini na tatizo la ajira. Tunalengo la kukuza uchumi kwa angalau 8% kwa mwaka na kutengeneza ajira zipatazo milioni 8,” amesema Rais John Magufuli
Baada ya hotuba hiyo iliyochukua takribani saa moja na nusu, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameahirisha bunge hadi Februari 2, 2021.
Katika mkutano huo wa kwanza uliomalizika leo, shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwa ni pamoja na kumchagua spika na naibu spika, kuthibitisha jina la waziri mkuu, wabunge wateule kula kiapo cha uaminifu na Rais kulifungua rasmi Bunge la 12.
Post Comment
Hakuna maoni
Chapisha Maoni