ELIMU YA MLIPA KODI NYUMBA KWA NYUMBA, MWAROBAINI MIGOGORO YA ARDHI
Bibi Nyamate Ligima kiongozi wa kikosi kazi maalum cha kutoa elimu ya kodi nyumba kwa nyumba akimuelimisha Bwn. Zuberi Miraji, mkazi wa mtaa wa Negamsi Halmashauri ya Mji wa Babati |
Wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Manyara wakitoa elimu nyumba kwa nyumba katika mtaa wa Negamsi (kwa masista) Halmashauri ya Mji wa Babati. |
Na. Eliafile Solla
Siku
ya elimu ya mlipa kodi ya pango la Ardhi imetajwa kuwa mwarobaini katika
utatuzi wa migogoro ra Ardhi hasa migogoro inayohusiana na mipaka ya viwanja
pamoja na ile ya upimaji juu ya upimaji. Hayo yamesemwa na Kaimu kamishna wa
Ardhi Msaidizi Mkoa wa Manyara Bwn Leonardd Msafiri alipokutana na kikosi kazi
maalum kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kutoa
elimu ya kodi ya pango la Ardhi pamoja na masuala mengine yahusuyo sekta ya
Ardhi katika Mkoa wa Manyara.
Akizungumza
katika utekelezaji wa zoezi hilo la utoaji elimu ya kodi nyumba kwa nyumba,
Msafiri alisema Wizara iligatua madara kwa maana ya kusogeza huduma karibu na
mteja kutoka kuwa na ofisi za Ardhi za kanda ambazo zilikuwa nane (08) nchi
nzima na kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa kwenye kila mkoa katika mikoa yote
26 ya Tanzania Bara.
Msafiri
alisisitiza kwamba, Wizara imepiga hatua kubwa kuanzisha kampeni ya siku ya
elimu ya mlipa kodi kwa sababu utoaji elimu nyumba kwa nyumba unawapa fursa ya
kukutana na wateja wao moja kwa moja na pia wanagundua changamoto nyingi na
tofauti tofauti wanazokutana nazo wananchi katika maeneo wanayomiliki.
Nae
Mkuu wa kitengo cha kodi kutoka Wizara ya Ardhi Makao makuu Dodoma Bwn Denis
Masami alisema, jukumu la msingi la wizara ni kupanga na kupima lakini hakuna
upangaji wala upimaji utaokuwa na tija kama wananchi watakuwa hawana elimu ya
kutosha kuhusu umuhimu wa kupimiwa na kupangiwa maeneo yao.
Masami
aliongeza kwamba, elimu inayotolewa sasa nyumba kwa nyumba ni fursa nzuri ya
kuboresha kumbukumbu za wamiliki kutokana na uhalisia kwamba Wizara imeboresha
taratibu nyingi za utoaji hudumu zikiwemo zile za ukadiriaji kodi ya pango la
Ardhi na ulipaji ambapo sasa zinafanyika kielektroniki.
Aidha
Zuberi Njola mkazi wa Mtaa wa Negamsi katika Halmashauri ya Mji wa Babati,
ambaye alifikiwa na watoa huduma katika mji wake alifurahia sana zoezi hilo na
kuiomba Wizara kuwafikia wengi zaidi.
‘Huu
ni mkakati mzuri, tulio wengi hatuzijui haki zetu za msingi hasa kuhusiana na
masuala ya Ardhi. Pia migogoro mingi tunaitengeneza wenyewe kwa sababu hatuna
uelewa wa mambo. Kutoa elimu nyumba kwa nyumba kama hivi kunaleta faraja kwetu
wananchi, tunaiomba Wizara iendeleze mkakati huu kwani tukishirikiana
hakutakuwa na migogoro alisema Zuberi’
Siku
ya elimu ya mlipa kodi ya Ardhi ni kampeni maalum iliyoanzishwa na Wizara ya
Ardhi, Nyumba, na Maendeleo ya Makazi ambapo kila siku ya Ijumaa watendaji wa
sekta ya Ardhi kote nchini hupita nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa kutoa elimu
kwa wamiliki wa Ardhi kuhusu sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayosimamia
sekta ya Ardhi.
-------------------------------------------MWISHO---------------------------------------------------------
Hakuna maoni
Chapisha Maoni