Rais Magufuli Akutana na Profesa Lumumba..... Kansela wa Ujerumani amtumia ujumbe
Rais
wa Tanzania, John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Msomi na
Mwanajumui wa Afrika (Pan-Africanist) Profesa Patrick Lumumba, Ikulu
Jijini Dar es Salaam.
Rais
Magufuli na Profesa Lumumba ambaye ni raia wa Kenya wamezungumzia
masuala mbalimbali yahusuyo juhudi za Afrika katika kuimarisha uchumi
kwa kutumia rasilimali zake .
Pia wajibu wa Waafrika na viongozi wao katika kuimarisha huduma za kijamii na kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Rais
Magufuli amempongeza Profesa Lumumba kwa juhudi zake za kueleza
waziwazi makosa yanayosababisha nchi za Afrika kubaki nyuma kiuchumi,
kijamii na kisiasa, wajibu wa viongozi na wananchi wa Afrika katika
kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi zao na mapenzi yake
makubwa kwa Afrika.
Rais
Magufuli amemueleza juhudi ambazo Serikali inazifanya katika kujenga
uchumi imara wa kujitegemea ikiwamo utekelezaji wa miradi mikubwa ya
kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa Bwawa la Nyerere
litakalozalisha megawati 2,115 za umeme na kuongeza usambazaji wa
umeme kutoka vijiji 2,018 hadi kufikia vijiji 8,587.
Pia,
ujenzi wa barabara na madaraja makubwa na madogo, kutoa elimu bila
malipo kwa shule za msingi na sekondari, kuongeza mikopo ya elimu ya
juu, kuongeza ukusanyaji wa mapato, kudhibiti rasilimali muhimu ya
madini na kupambana na rushwa.
“Mimi
sijawahi kukutana nawe kabla, lakini nakusikia na kukuona kupitia
vyombo vya habari jinsi unavyopaza sauti kuhusu Bara la Afrika,
nakupongeza kwa juhudi hizo, na ninafarijika kwamba unaisemea vizuri
Afrika,” amesema Rais Magufuli.
Kwa
upande wake, Profesa Lumumba amemshukuru Rais Magufuli kwa kutenga muda
wake kuzungumza naye na amempongeza kwa juhudi kubwa alizozionesha
katika kipindi kifupi cha uongozi wake wa miaka minne ambapo ameonyesha
mfano wa namna ya kupigania rasilimali za nchi ikiwemo madini, kujenga
nidhamu ya utumishi Serikalini, kuimarisha uchumi, kupambana na wizi wa
mali za umma, rushwa na ufisadi.
Profesa
Lumumba amesema inafaa kwa nchi za Afrika kujifunza mambo yanayofanyika
Tanzania kwa sasa na amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Waafrika kujiamini
na kuchukua hatua madhubuti za kuwaondoa katika hali ya sasa ambapo
rasilimali zake zinachukuliwa na Mataifa ya nje ilihali wananchi wake
wakikabiliwa na changamoto mbalimbali.
Wakati huo huo,
Rais Magufuli amekutana na Mwakilishi wa Kansela wa Ujerumani
anayeshughulikia masuala ya Afrika, Guenter Nooke, Ikulu Jijini Dar es
Salaam.
Nooke
amewasilisha ujumbe wa Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na pia
ameelezea kufurahishwa kwake na hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa
hapa nchini ikilinganishwa na alipokuja miaka iliyopita.
Pia
amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali katika kupambana na rushwa
na kuimarisha uchumi ambapo ameahidi kuwa Ujerumani itaendelea
kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji na biashara na masuala mengine
ya kijamii.
Kwa
upande wake, Rais Magufuli amemhakikishia Kansela wa Ujerumani kuwa
Serikali ipo tayari kuuendeleza na kuukuza zaidi uhusiano mzuri na wa
kihistoria uliopo kati yake na Ujerumani, na inawakaribisha
wafanyabiashara na wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini.
Katika mazungumzo hayo, Nooke ameongoza na Balozi wa Ujerumani hapa nchini Regine Hess.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni