Zinazobamba

WABUNGE WA CHADEMA SASA WAMCHARUKIA MTEULE WA MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA

WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamezidi kumkaba koo Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexunder Mnyeti baada ya leo kuwasilisha ushahidi zaidi wa video unaoonyesha akiwashawishi Madiwani wa chama hicho kuhama, anaandika Faki Sosi.
Leo ni mara ya pili wabunge hao kuwasilisha ushahidi wa video kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)
Oktoba 2 mwaka huu, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), akiongozana na wabunge wenzake aliwasilisha ushahidi Takukuru.
Wabunge aliongozana nao siku ya kwanza ni Mchungaji Peter Msigwa ambaye ni Iringa mjini na Godbless Lema wa Arusha mjini wote kutoka Chadema.
Video hiyo inaonyesha Mnyeti na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Arumeru wakiwashawishi Madiwani wa Chadema kukubali kuhama chama hicho.
Wateule hao wa Rais wanadaiwa kuwashawishi Madini hao kukubali kuhama kwa ahadui kwamba watapatiwa nafasi za ajira kulingana na elimu walizonazo.
Leo Nassari akiongozana na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea wamefika Takukuru wakiwa na Flash yenye ushahidi na kuikabidhi kwa ajili ya uchunguzi.
Nassari ameeleza kuwa wamerejea tena Takukuru kuwasilisha ushahidi mwingine huku akisema ni ngumu ‘kesi ya Ngedere kumpelekea Nyani’
Amedai kwamba licha ya kuwasilisha ushahidi huo, Mnyeti amekuwa akijigamba kuwa yeye ni swahiba wa Rais na kwamba hataweza kuathirika chochote.
“Kwa mara ya kwanza tumeweza kuwasilisha ushahidi usiokuwa na shaka… na kwamba sasa Takukuru wapeleke mahakamani sisi ushahidi wetu umekamilika ni jambo la aibu kuwaona watumishi wale kuwepo ofisini”, amesema
Kwa upande wake, Kubenea ambaye yupo kwenye kamati ya Tamisemi ameeleza kuwa ameshiriki katika kazi ya kukusanya ushahidi huo.
Kubenea amesema kuwa tayari wao wamekamilisha ushahidi wao na kusisitiza kuwa kesi hiyo ipelekwe mahakamani mapema.
Ameshangazwa kuwaona watuhumiwa bado wapo ofisini badala ya kukaa pembeni ili kupisha uchunguzi wa Takukuru.