Zinazobamba

MAWAZIRI WA MAGUFULI WAANZA KAZI NA MIKWALA BAADA YA KUAPISHWA,SOMA HAPO KUJUA


Waziri, George Mkuchika amefunguka na kuweka wazi mipango yake katika kutumikia nafasi yake na kusema yeye ataanza kuhakikisha watumishi wa Umma wanatumia muda wao kufanya kazi na hataki kusikia watumishi wameondoka makazini kwenda kunywa chai.

Waziri Mkuchika ambaye leo Oktoba 9, 2017 ameapishwa na Rais Magufuli kuwa Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema kuwa katika kipindi chake atahakikisha wafanyakazi wanalipwa mshahara kulingana na kazi zao kweli, na wanatumia muda wa kazi kufanya kazi za serikali.

“Kwanza katika kipindi changu nikiwa Waziri kwa watumishi wa Umma, nataka wananchi wanapofika maofisini wawakute maofisini, mara nyingi wengi wanaripoti ofisini baada ya muda wanaondoka wanasema wanaenda kunywa chai, yaani wananchi wanatoka vijijini wanamsuburi mtumishi aje eti ameenda kunywa chai jambo hili kuanzia leo nitasimamia kuhakikisha watumishi wa umma wanashinda kazini kwao ili kila mtumishi wa Umma alipwe mshahara kwa kufanya kazi muda wote” amesema Mkuchika.

Aidha Mkuchika amesema kuwa kwa sasa watumishi wengi wa Umma wanalipwa mshahara kamili kwa kufanya kazi robo za serikali jambo ambalo yeye atakwenda kulisimamia na kuhakikisha kuwa watumishi hao wanafanya kazi kamili ili walipwe kulingana na kazi zao kamili.

Mbali na hilo Mkuchika amedai kuwa atakwenda kuongea na Waziri wa Elimu ili ikiwezekana somo la Rushwa lianze kufundishwa kuanzia shule ya awali nchini mpaka vyuo vikuu na kusema watu wamekuwa wakichukua na kutoa rushwa kwa kuwa hawana elimu ya kutosha juu ya athari ya rushwa.

JAFFO NA KIGWANGALLA NAO HAKUWA NYUMA ,SOMA

Aliyekuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, Seleman Jafo baada ya kuteuliwa na kuapishwa kuwa Waziri wa wizara hiyo amewaahidi Watanzania kuwa wategemee utendaji mzuri wa kazi kutoka kwake huku akiwaomba watumishi wote umma kufanya kazi kwa spidi.

Wakizungumza Ikulu jijini Dar es salaam mara baada ya kuapishwa, Mhe Jafo amesema lengo lake ni kuisukuma nchi ifikie malengo yanayotarajiwa huku Dkt Kigwangalla akisema Mh. Rais ameonyesha imani kubwa sana na uwezo wake.

“Kikubwa zaidi niwaahidi Watanzani wategemee utendaji mzuri wa kazi, lakini niombe sana watumishi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lazima wajipange kufanya kazi kwa bidii , Wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, Wakurugenzi naomba waongeze spidi na Wakurugenzi waongeze spidi lakini watumishi wote waongeze spidi lengo ni tuisukume nchi yetu ifike katika malengo tunayoyatarijia

Hata hivyo Mhe. Jafo alipoulizwa kuwa ikiwa ni miongoni mwa Waziri walipandishwa yeye anafikiri ni kwanini kapandishwa na kuwa Waziri kamili? Akajibu “Ni mipango ya mwenyezi Mungu jambo la kwanza, la pili ni imani ya Mheshimiwa Rais kwangu, tatu ni utendaji wa kazi kwasababu ni lazima popote utakapo niweka ni lazima nifanye kazi kwasababu nina dhamana ya Watanzania naamini popote Mungu ananiona.”

Kwa upande wake aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya ambaye kwasasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla amesema kuwa “nimefarijika sana pia nimepewa imani kubwa na Mhe. Rais, nimepewa Wizara nyeti ni wizara ambayo inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa ni wizara nyeti sana, na mimi kupewa jukumu hili maana yake mhe. Rais ameonyesha imani kubwa sana na uwezo wangu lakini pia na uzalendo nilionao naomba niwaambie Watanzania na Mhe. Rais Kuwa sitawaangusha.”