DAMU YA TUNDU LISSU YAMLAZA SHEIKH PONDA LUPANGO ,SOMA HAPO KUJUA
MWANAWAZUONI, mwanaharakati na kiongozi mashuhuri wa madhehebu ya dini ya Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, bado anaendelea kushikiriwa na jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, anaandika Faki Sosi.
Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo na zilizomnukuu Sheikh Rajabu Katimba zinasema, Sheikh Ponda ambaye aliripoti polisi leo asubuhi, bado anaendelea kuhojiwa akituhumiwa kufanya uchochezi.
Sheikh Ponda aliwasili Kituo kikuu cha Polisi Kati (Centro), majira ya saa nne asubuhi leo Ijumaa, akiwa ameongoza na mawakili wake watatu, akiwamo Prof. Abdallah Safari.
Kwa mujibu wa Sheikh Katimba, miongoni mwa mashitaka anayotuhumiwa Sheikh Ponda, ni madai kuwa ametaka wananchi kutoogopa vyombo vya dola na kuituhumu serikali kuhusika na vitendo vya mauaji kwa raia nchini.
Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alishambuliwa kwa risasi za moto Alhamisi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika,” majira ya saa saba na nusu mchana wa tarehe 7 Septemba mwaka huu.
Shambulio dhidi ya Lissu ambaye ni rais wa chama cha wanasheria nchini, Tanganyika Low Society (TLS), Mnadhimu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni, mwanasheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, lilifanyika nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma. Alikuwa akirejea nyumbani kutokea bungeni.
Lissu alinusurika kifo, wiki mbili baada ya kunukuliwa akisema, “maisha yangu yako hatarini.”
Habari zinasema, kwa sasa hali ya Lissu ambaye amelazwa kwenye hospitali kuu ya Nairobi nchini Kenya anakopata matibabu ya majeraha ya risasi inaendelea vizuri na Sheikh Ponda alipata fursa ya kukutana na kuzungumza naye kwa kina.
Uongozi wa jeshi la polisi ulianza kumtafuta Sheikh Ponda tokea juzi Jumatano, mara baada ya kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika kwenye hoteli ya Iris, Kariakoo, jijini Dar es Salaam ambako alieleza alichoita, “mazungumzo yake na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, alinusurika kukamatwa na jeshi hilo katika mazingira ambayo wengi yamewaacha midomo wazi, baada ya polisi kufika eneo hilo, dakika chache baada ya yeye “kusepa.”
Kufuatia kushindwa kumtia mbaroni, jana (Alhamisi) Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, alimtaka Sheikh Ponda kujisalimisha mwenyewe kwa jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, siku moja baada ya kurejea nchini akitokea Nairobi, Sheikh Ponda alisema, “nimeguswa na maneno ya Lissu. Kwamba tusiogope na kuwa damu yetu iliyomwagika, haitakwenda bure.”
Sheikh Ponda amesema, “tulipokuwa tunabadilisha mawazo, niliguswa na hisia kubwa, badala ya mimi kumpa matumaini yeye ndiye aligeukwa na kunipa matumaini.”
Amesema alikwenda Nairobi kumjulia hali Lissu, kumwombea dua, kumjengea matumaini ya afya na kujenga mazingira mapana yanayotosha kulizungumza jambo lililomfika.
Kwa mujibu wa Sheikh Ponda, Lissu alimwambia: “Wewe (Sheikh Ponda), ulipingwa risasi na ukapelekwa gerezani na kidonda kinachululiza damu. Mimi nimeshambuliwa kwa makumi ya risasi. Damu nyingi imemwagika.
Lakini nakuahidi sheikh wangu, damu yetu haitamwagika bure. Bali, itakuwa chachu ya ushindi.”
Ameongeza, “Lissu amehimiza mshikamano na alionyesha ana matumaini na Watanzania kwa harakati wanazozifanya. Tunamuombea arudi nchini kuendelea na majukumu yake.”
Kwa takribani miaka 25 sasa, Sheikh Ponda amekuwa akifahamika kama mwanaharakati wa kutetea “haki za waislamu.”
Alianza mapambano hayo, mwaka 1993 alipounda taasisi yake, akijikita katika kuita serikali iwachukulie hatua watuhumiwa wa mauwaji yaliyotokea kwenye Msikiti wa Mwembechai jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba zake kaadhaa, Sheikh Ponda amwekuwa akifanya marejeo katika historia ya nchi kabla na baada ya uhuru.
Taarifa za hizi sasa zinasema muda huu, polisi wanaenda kumpekua nyumbani kwake na ofisi kwake.