Zinazobamba

KITUO CHA MABASI UBUNGO KUZALISHA AJIRA 20,000

IMG_5698
Meneja Mkuu wa Ksmpuni ya Linghang,Cathy Wang kutoka jiji la Shanghai China walipotembelea Ofisi ya Meya wa Dar es salaam Isaya Mwita.
IMG_5676
Meya wa Jiji la Dar es salaam Isaya Mwita akiwa na wageni kutoka China walipomtembela Ofisini kwake wakiwa kwenye picha ya pamoja.
IMG_5710
Wageni kutoka jiji la Shanghai nchini China wakiwa katika picha ya pamoja huku wakionesha bendera ya Taifa la nchi yao walipotembelea Ofisi ya Meya wa Dar es salaam.
IMG_5689
Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita akiwa katika picha ya pamoja.

MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amekutana na ugeni kutoka Jiji la Shanghai nchini China na kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo jijini hapa ikiwemo suala la uboreshaji wa Kituo cha Mabasi Ubungo.
Ugeni huo uliambatana na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Linghang Group, Cathy Wang ambayo imeingia mkataba na halmashauri ya jiji kwa ujenzi wa kituo hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo, Meya Mwita alisema kuwa ugeni huo umeridhia kuwekeza katika nyanja mbalimbali ikiwemo Kituo cha Mabasi Ubungo.
Alifafanua kuwa Jiji la Dar es Salaam linakaribia kuanza kwa ujenzi wa mradi mkubwa wa kubadilisha Kituo cha Mabasi Ubungo na kwamba hatua mbalimbali zimeshakamilika ili kupisha mradi huo.
Alisema kuwa mara baada ya kukamilika kwa mradi huo jumla ya Watanzania 20,000 watapata ajira jambo ambalo litawezesha kuongeza kipato kwa wananchi na hivyo pia kuwezesha vijana kuondokana kwenye makundi ambayo sio salama.
Alisema kufanikishwa kwa mradi huo, utasaidia pia kuongeza mzunguko wa fedha jijini hapa kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi za kibiashara.
“Leo nimekutana na ugeni ambapo kwa kiasi kikubwa mnafahamu ndugu zetu hawa wamekuwa na urafiki mkubwa katika nchini yetu, tumejadiliana mambo mengi ambayo yote ni ya kuleta maendeleo katika jiji letu.
“Lakini kubwa zaidi ni kuhusu ujenzi wa Kituo cha Mabasi Ubungo, ambapo hivi karibuni tunatarajia kuanza kwa mradi huo, na wananchi pia watajulishwa, nitumie fursa hii kuwaeleza wananchi kuwa jiji linafuata utaratibu katika kutekeleza mradi huo,” alisema Meya Mwita.
“ Fursa hii ni kubwa ambayo tumeipata, Watanzania watapata ajira, mzunguko wa fedha kwenye jiji letu utaongezeka, kama meya wa jiji hili nimewakaribisha tufanye kazi pamoja, lengo likiwa ni kuweka jiji kwenye muonekano mzuri,” aliongeza.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Linghang, Cathy Wang alimpongeza Meya Mwita kutokana na aina ya utendaji wake wa kazi na kuahidi kuonyesha ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo.
Alisema kuwa Meya Mwita ni kiongozi anayefanya kazi kwa bidii na umakini na kwamba kutokana na jitihada hizo za kulijenga jiji , kampuni yao itafanya  kazi na kumhakikishia kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.