DAREVA WA TUNDU LISSU NA VISENT MASHINJI WANASAKWA NA JESHI LA POLIS,SOMA HAPO KUJUA
Wakati Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi, Kenya, Jeshi la Polisi limemtaka dereva wake, Adam na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji kuripoti Polisi Dodoma au Makao Makuu ya Upelekezi Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, SACP, Giless Muroto alisema jeshi hilo linamtaka devera wa Lissu na Katibu Mkuu wa Chadema kuripoti polisi ili kufanya mahojiano nao.
“Popote alipo dereva wa Lissu, Adam ajitokeze na afike Polisi Dodoma na Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam ili kutoa maelezo kuhusiana na tukio kwani ndiye alikuwa pamoja na majeruhi,” alisema.
Kamanda alisema kitendo cha kutoweka kwa dereva huyo na kujificha ni kosa la jinai na kama kuna mtu au watu wanaomficha, wanatenda kosa la jinai, wamfikishe Polisi mara moja bila kukosa kwa kuwa ni shahidi muhimu katika upelelezi.
Kuhusu Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Mashinji, naye anatakiwa kuripoti kituo cha polisi kutokana na hotuba aliyotoa juzi, ambayo iliwahamasisha wanachama wa chama hicho popote walipo, kuwa wanatakiwa kuchangia damu, kitendo ambacho ni uchochezi, na kinaamsha mshituko katika jamii.
Akizungumzia upepelezi kuhusu Lissu kushambuliwa na risasi kati ya 28 hadi 32 na tano kumdhuru, Kamanda alitoa mwito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi.
Kamanda Muroto alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na timu ya upelelezi kutoka Makao Makuu ya Upepelezi kutoka Dar es Salaam, linaendelea kufanya upelelezi wa kina ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo.
“Pia taarifa zimetolewa mapema katika wilaya na mikoa jirani ili kufanya misako na ufuatiliaji kulingana na taarifa zilizopo ndani ya jeshi hilo,” alisema.
Wakati upelelezi ukiendelea, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa sahihi ili kufanikisha kuwabaini watu waliohusika na tukio hilo la kumshambulia Lissu na matukio mengine.
Kamanda pia aliwaonya wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuandika habari za upotoshaji, uchochezi dhidi ya taasisi za serikali na baadhi ya viongozi wa dola kuhusu tukio hilo, kuacha mara moja.
Alitoa angalizo kwamba wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii, wanatenda kosa kisheria waanze kuchukua tahadhari wasije tumbukia mikononi mwa sheria.
Aliwataka wale wote wenye taarifa sahihi kuhusu tukio hilo la kushambuliwa Lissu wajitokeze na watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi au kwa viongozi wa serikali walipo na taarifa hizo zitafanyiwa kazi ili kukomesha vitendo hivyo.
Aidha alisema jeshi hilo limeyakamata magari manane aina ya Nishani Patrol na yanafanyiwa uchunguzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na taasisi nyingine kuhusiana na kuhusishwa na tukio la kujeruhiwa kwa risasi Mbunge Lissu.
Lissu ambaye ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alishambuliwa kwa risasi Septemba 7, mwaka huu saa 7.30 Area D katika maghorofa ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika Manispaa ya Dodoma.
Uchunguzi wa awali kuhusu tukio hilo, ambalo watu walioshambulia hawajulikani, Kamanda Muroto alisema unaonesha kuwa wahalifu walikuwa na silaha ya SMG/SAR kutokana na maganda ya risasi yaliyokutwa eneo la tukio.