Zinazobamba

CUF YA MAALIM SIEF YAWAPONGEZA WABUNGE WA UKAWA KWA KUWASUSIA WABUNGE WA LIPUMBA,SOMA HAPO KUJUA




CHAMA cha Wananchi (CUF) upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad umeupongeza uamuzi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kususia kuapishwa wabunge wapya wa viti maalumu wa chama hicho.
Wabunge walioapishwa juzi wanachukua nafasi za wenzao waliofukuzwa uanachama na Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiani wa CUF,  Mbarala Maharagande alisema bado wanawatambua wabunge wanane waliovuliwa uanachama na kupoteza ubunge.

“Wabunge hawa walioapishwa jana (juzi)  wamekubalika ili kuingiza upinzani bandia ndani ya CUF na upinzani kwa ujumla. Hatutakubali kutumiwa katika kutengeneza upinzani ‘feki’ wa kisiasa ili kukisaidia CCM kuendelea kubaki madarakani,” alisema.

Amesema kitendo cha kuapishwa wabunge hao kimeshusha haiba ya Spika Job Ndugai kuongoza Bunge ambalo ni mhimili Dola unaopaswa kuwa alama ya uadilifu katika nchi.

Amesisitiza kuwa CUF kupitia Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kitaendelea kuwatambua wabunge na madiwani wawili wanaodaiwa kuvuliwa uanachama, kusisitiza kuwa bado wanawatambua kama wanachama wao.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa wabunge wa CUF, Riziki  Mngwali amesema anasikitishwa na hujuma zinazofanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Uchaguzi (NEC) na Bunge ili kuihujumu CUF licha ya kuwa taasisi hizo zipo kwa ajili ya kusimamia demokrasia nchini.

“Inasikitisha nchi iliyojengwa kwa mfumo wa kidemokrasia na taasisi hizi zikipewa mamlaka ya kuisimamia, lakini badala yake ndiyo zinafanya hujuma dhidi ya Chama cha CUF,” alisema Mngwali.
Wabunge walioapishwa juzi ni Alfredina Kaigi, Kiza Mayeye, Nuru Bafadhili, Rukia Kassim, Shamsia Mtamba, Sonia Magogo na Zainab Amir.

Waliovuliwa uanachama ni Severina Mwijage, Saumu Sakala, Salma Mwassa, Riziki Mngwali, Raisa Mussa, Miza Haji, Hadija Ally Al-Qassmy na Halima Mohamed.