Serikali imekipatia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) zaidi ya Sh. bilioni 6.7, SUMATRA YAKIPIGIA MFANO
Serikali imekipatia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)
zaidi ya Sh. bilioni 6.7 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya
ufundishaji wa chuo hicho, ikiwemo kujenga madarasa na nyumba za walimu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Zacharia Mganilwa alisema fedha hizo
ambazo zimetengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha zitasaidia kufanya
NIT itoe wataalam wenye weledi wa kushindana katika soko la kimataifa
la ajira.
Prof. Mganilwa alisema chuo kimejipanga pia kuendelea kutoa
wataalam waliobobea katika fani mbalimbali ambazo zitaendana na
mahitaji ya sasa ya taifa na kushiriki katika shughuli za ujenzi wa
taifa, ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta kati ya Uganda na Tanzania,
upanuzi wa bandari na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.
“Chuo kinatoa mafunzo katika mfumo unaotambulika na Baraza
la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na mfumo unaozingatia elimu kwa
vitendo ambao unampa uwezo mkubwa mwanafunzi kushindana katika soko la
ajira,” alisema Prof. Mganilwa.
Alisema Chuo hicho kinadahili wanafunzi waliofaulu kidato
cha nne kwa masomo ya cheti na diploma na wanafunzi waliomaliza kidato
cha sita kwa masomo ya shahada.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa
Majini na Nchikavu (Sumatra), Giliard Ngewe alisema NIT ni muhimili wa
uchumi na kwamba bila usafirishaji huo uchumi hauwezi kukua.
Ngewe alisema wakati wa awamu ya kwanza ya Serikali
kulikuwa na mashirika ya usafirishaji ya mikoa ambayo yalichangia kwa
kiasi kikubwa katika kujenga uchumi wa taifa, ambayo "yaliongozwa na
wataalamu kutoka chuo hiki".
Akizungumza katika hafla hiyo, rais wa serikali ya
wanafunzi wa NIT, Stambuli Mwombeki alipongeza juhudi zinazofanywa na
Rais John Magufuli ya uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji na
kwamba vijana wanaohitimu katika chuo hicho wataweza kupata ajira katika
sekta hizo.
Alisema miongoni mwa mafunzo yanayotolewa chuoni hapo ni
uhandisi wa vyombo vya usafiri wa anga, utalaamu wa usafirishaji wa njia
ya reli ambayo inaboreshwa na kuwa ya kiwango cha kisasa pamoja na
urubani na huduma za denge.
Chanzo: Nipashe