PROFESA MUKANDALA KUKIONA,MWANAFUNZI WAKE AMBURUZA MAHAKAMANI,SOMA HAPO KUJUA
ALIYEKUWA mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaa, Alphonce Lusako, amemburuza mahakamani, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala akimtuhumu kumkatisha masomo bila kufuata utaratibu, anaandika Hellen Sisya.
Mukandala anatuhumiwa kutumia madaraka yake vibaya na kumfukuza chuo Lusako ambaye inadaiwa alifukuzwa chuoni hapo pasipo kufuata taratibu za kisheria.
Katika kesi hiyo ya madai namba 71 ya mwaka 2017 ambayo imetajwa leo hii mbele ya Hakimu Oswad wa mahakama ya wilaya Kinondoni jijini Dar es salaam .
Lusako anaiomba mahakama itoe adhabu kwa Profesa Mukandala pamoja na chuo hicho ya kumlipa Sh. millioni 600 kama fidia kwa kuwa wamemshushia heshima katika jamii pamoja na kumkosesha nafasi ya kupata elimu tangu mwaka 2012.
Mbali na kiasi hicho cha pesa, Lusako pia anawadai fidia ya Sh millioni tano, kwa ajili ya gharama zote ambazo alizotumia kwa ajili ya ada pamoja na pesa ya matumizi binafsi akiwa chuoni hapo tangu mwaka jana mwishoni mpaka mapema mwaka huu alipofukuzwa.
Kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Septemba 7 mwaka huu ambapo Lusako anawakilishwa na wakili msomi Seka John na kwa upande wa Profesa Mukandala pamoja na chuo wanawakilishwa na wakili msomi Zabibu Abdalaah.
Lusako alifukuzwa chuoni hapo kwa mara ya kwanza mwaka 2012 akituhumiwa kufanya kosa la kinidhamu ambapo baada ya kukaa nyumbani kwa takribani miaka mitano, hatimaye October mwaka jana alifanikiwa tena kupata nafasi ya kuendelea na masomo yake ya elimu ya juu chuoni.
Alikuwa akisoma shahada ya sheria, lakini mapema mwaka huu chuo hicho kilimfukuza tena kwa mara ya pili kwa madai kuwa alikuwa amedahiliwa chuoni hapo kimakosa.