Zinazobamba

MBUNGE KUBENEA AMJIBU JERRY MURO,SOMA HAPO KUJUA

NIMESOMA kilichoitwa na Jerro Muro, “ushauri kwa wanasheria nchini ” juu ya msimamo wao wa kutohudhuria mahakamani leo (Jumanne) na kesho, anaandika Saed Kubenea.
Hatua ya mawakili hao, imefuatia kuvamiwa na kulipuliwa kwa ofisi ya mawakili wenzao jijini Dar es Salaam, maarufu kwa jina la IMMA Advocates.
Ofisi za IMMA zililipuliwa usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika.”
Mawakili kupitia chama chao – Tanganyika Law Society – wameamua kutokwenda mahakamani ili kupinga uvamizi na “kuombeleza” pamoja na wenzao.
Kwa mujibu wa tamko lililotolewa na Baraza la Uongozi la TLS, uamuzi wa kutohudhuria mahakamani unalenga kupeleka ujumbe kuwa mawakili wanahitaji kufanya kazi zao bila vitisho.
Baraza linasema, usalama wa mawakili ndio usalama wa wannachi wengine wote. Kwamba mawakili hawezi kufanya kazi za utetezi kwa uhuru.
Lakini Jerry Muro anapinga maamuzi hayo. Anasema, TLS imekosea kuchukua hatua hizo na kwamba chombo hicho kinatumika kisiasa.
Kwa tunaomfahamu vema Jerry Muro, hatukutarajia kuwa angetoa kauli ya kupinga uamuzi huu. Tulitarajia angekuwa mtu wa mwisho kufanya hivyo.
Hii ni kwa sababu, Jerry ni mmoja wa wanufaikaji wakubwa wa uhuru wa mawakili nchini.
Jerry anajua kuwa kama mawakili wasingekuwa huru, leo hii asingekuwa uraiani. Angeshafungwa.
Kesi yake ya kupokea rushwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, miaka mitatu iliyopita isingemuacha salama, kama mawakili wasingekuwa huru.
Jerry anajua, kama sisi wengine tujuavyo, kwamba aliomba rushwa na alikula rushwa. Jerry anajua jinsi kulivyokuwa na mashinikizo kutoka pande zote za kutaka kumtia hatiani.
Lakini mawakili hawakujali kama Jerry Muro amekula rushwa au hakula, badala yake, waliamua kusimama kidete kumtetea.
Ni kwa sababu, maadili yao yanaelekeza kutoa fursa kwa kila mtu kuwa na haki ya kutetewa mahakamani.
Aidha, kwa minendo ya Jerry ya sasa na ambayo ilianza siku chache kabla ya kukamatwa na rushwa, ndugu huyu hana sifa, hadhi wala uwezo wowote wa kutoa ushauri kwa mawakili ama kwa taaluma hiyo adhimu.
Kwa siku za hivi karibuni, taaluma ya mawakili ndio pekee iliyosalia kwenye msimamo wake wa kutetea haki za wananchi.
Kwa msingi, ni vema mawakili mkapuuza vijineno vya watu aina ya Jerry Muro wanaofanya kazi kwa maslahi ya matumbo yao.
Mawakili muendeele kulinda heshima yenu. Uvamizi wa mmoja wenu, ni uvamizi kwenu wote.