LHRC yawafariji akina mama Muhimbili
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamefanya ziara katika Wodi ya
Wanawake, Hospitali ya Taifa Muhimbili kuadhimisha Siku ya Mwanamke wa
Afrika pamoja na wanawake hospitalini hapo.
Wafanyakazi
na uongozi wa LHRC waliadhimisha Siku ya Mwanamke wa Afrika ambayo
huadhimishwa Julai 31 kwa kutimiza wajibu wa kijamii wa kuwatembelea
wanawake hospitalini hapo na kuwafariji huku wakiwapa zawadi mbalimbali.
Akizungumza
na vyombo vya habari hospitalini hapo, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu, Bi. Anna Henga alisema “Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kimeona ni vyema kuadhimisha Siku ya
Mwanamke wa Afrika kwa kuzuru Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili
kuonesha umuhimu wa sekta ya afya na kuikumbusha serikali na wadau
wengine wa sekta hiyo umuhimu wa kufanya juhudi za makusudi katika
kupambana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo hapa nchini”.
Kwa
mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania, 2016 inayotolewa na
Kituo hicho, sekta ya afya imekumbwa na changamoto kadha wa kadha ambazo
zinahatarisha haki ya msingi ya wananchi kupata huduma bora za afya.
Changamoto tajwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa wafanyakazi katika
sekta ya afya, takwimu zikionyesha upungufu wa asilimia 51; sambamba na
vituo vya afya takribani 2000 kuwa na wafanyakazi wasio na sifa huku
kukiwa na wahitimu takribani 20,000 wenye sifa ambao hawajapatiwa ajira.
Pia, Ripoti hiyo; imebainisha uwepo wa changamoto ya upatikanaji wa
dawa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti iliyopangwa
kwa ajili ya manunuzi ya dawa muhimu ambapo Bohari Kuu ya Dawa (MSD)
ilikuwa na upungufu wa asilimia 47 ya dawa muhimu.