HAMAD RASHIDI WA CHAMA CHA ADC AMVAA MAALIM SEIF,SOMA HAPO KUJUA
MWENYEKITI Chama Cha Alliance For Democratic Change (ADC) Hamad Rashid amewataka viongozi wa Chama cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Saif kumaliza mgogoro kwa vikao badala ya kusubiri kesi zilizoko mahakamani.
Kauli hiyo ameitoa leo akizungumza na viongozi na wanachama wa ADC katika maazimisho ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa chama hicho, amesema mahakama kazi yake ni kuhukumu tu lakini mgogoro utamalizika kwa njia ya mazungumzo.
“Ushauri wangu wamalize matatizo yao kwa vikao na mazungumzo, mahakama haiwezi kumaliza mgogoro bali inatoa hukumu tu, wao wamekuwa kila wanapokaa vikao ni kufukuzana,” alisema Rashid.
Aidha amemshutumu Maalim kuwa ni chanzo cha mgogoro huo kwani amekuwa hataki kusamehe na kuyamaliza hadi kufikia hatua ya kumuwekea chuki Profesa Lipumba kwamba hawezi hata kumpa mkono.
Rashidi ameongeza kwa kusema kuwa amekuwa mtu mbinafsi ambaye anatataka analoamuwa yeye liwe pasipo kusikiliza ushauri wa wengine. Kutokana na hali hiyo Rashid amesema hataki viongozi wa jinsi hiyo ndani ya chama chao.
Amesema kufanya siasa kunahitaji mtu mwenye hekima na busara ambapo alibainisha kuwa mwanasiasa mzuri ni yule mwenye mbinu na mikakati mizuri isiyo na vurugu.
Kwa upande mwingine amewataaka CUF- Maalim kuacha kueneza propaganda kuwa yeye ni msaliti na kwamba ADC ni CCM “B” huku akibainisha kuwa Maalim ndiye msaliti kwani haiwezekani kufanya mazungumzo na CCM peke yake bila kuwepo mashahidi wakujua kinachozungumzwa kisha kukaa kimya.