Zinazobamba

Askofu Malasusa aongoza ibada kuliaga kanisa litakalokumbwa na bomoabomoa

“Kwaheri kanisa letu.” Ndiyo maneno yaliyokuwa yakisemwa na waumini wa Usharika wa Kibamba wakati Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa akiwaongoza waumini wa kanisa hilo katika ibada ya mwisho jana, kabla ya kanisa hilo kubomolewa.

Kanisa hilo ni moja ya nyumba zaidi ya 30 za ibada zitakazokumbwa na bomoabomoa kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro kuanzia Kimara mpaka Kiluvya jijini Dar es Salaam.

Askofu Malasusa aliwataka waumini wa kanisa hilo kuwa na amani na kumshukuru Mungu kwa yote.

Alisema hayo wakati wa ibada ya kuondoa wakfu katika kanisa hilo ikiwa ni kutii agizo la Serikali.

Dk Malasusa alisema waumini hawana budi kumshukuru Mungu kwa kuwa jambo lolote hata likiwa baya linapotokea linakuwa na makusudi yake.

“Najua mna huzuni, majengo mengi yataondolewa na Serikali ili kupisha ujenzi wa barabara, kwa hili hamna budi kukubali na kuamini kuwa hiyo ni baraka kutoka kwa Mungu, zaidi kuweni na amani, ombeni baraka na mshukuruni Mungu,” alisema.

Alisema siku zote Mungu ana makusudi kwa kuwa palipo na huzuni huleta furaha na amani na tayari amewaonyesha kwa kuwabariki kupata eneo jingine kubwa ambalo wameanza ujenzi.

“Vitabu vya Mungu vinasema tusikate tamaa. Naomba msikate tamaa, pale akili ya binadamu inapoishia ndipo Mungu huanzia kutengeneza upya, jipeni moyo muwe na amani,” alisema.

Askofu huyo wakati akiondoa wakfu aligonga nyundo tatu ukutani ikiwa ni ishara ya kuhamisha agano na nyundo tatu sehemu ya madhabahuni huku nyingine tatu upande wa meza ya neno la Mungu.

Baada ya kumaliza kufanya hivyo, waumini na askofu huyo walitoka ndani na alizungumza nao na kuwataka wakamilishe haraka ujenzi wa kanisa jingine.

“Mungu atatenda, tayari amekwishatenda. Naomba ujenzi ukamilike haraka, nyundo hii niliyowakabidhi msiende kuiweka tu ikafanye kazi,” alisema Malasusa, ambaye amewahi kuwa Mkuu wa KKKT.

Hata hivyo, baada ya kuondoa wakfu waumini walitoka nje na kubeba baadhi ya vitu vilivyokuwa ndani ya kanisa na kuliaga kwa kunyoosha mkono wa kwaheri.

Waumini hao ambao waliliaga kanisa lao kwa huzuni wakionyesha ishara ya mkono baada ya kuambiwa na askofu kufanya hivyo, walisema hawana budi kuondoka japokuwa wanaona huzuni kwa kuwa walilizoea na kuliona kama makazi yao.

“Najisikia vibaya ila nimefarijika baada ya kanisa kutafuta eneo jingine. Pia, tunaheshimu mamlaka za Serikali, hivyo hatuna budi kuondoka,” alisema muumini wa kanisa hilo, Stephen Mollel.

Katibu wa Baraza la Wazee wa kanisa hilo, Aisimbo Natai alisema hawana budi kumshukuru Mungu.

“Tumeamua kuondoka kwenda jengo jingine ambalo tumeshaanza ujenzi ili kupisha agizo la Serikali kwa utaratibu wa kanisa. Kwa sasa jengo hili hatuna mamlaka nalo tena, Serikali wanaweza kuja kufanya shughuli zao,” alisema Natai.

Aliongeza kuwa ubomoaji wa kanisa hilo utafuata baadaye, lakini kwa sasa wameondoa agano na kuhamisha baadhi ya vifaa.

Akisoma historia fupi ya kanisa hilo mbele ya askofu, mwenyekiti wa ujenzi wa kanisa jipya, Praygod Chao alisema lilianzishwa mwaka 1975 likiwa na washarika 15 ambao awali waliungana na makanisa ya Anglikana na Katoliki kusali kwa zamu katika majengo ya Shule ya Msingi Kibamba.

“Mwaka 1976 baadhi ya wazee wa madhehebu haya matatu walikutana na kuzungumzia uwezekano wa kupata eneo la kuabudia, walimshirikisha mwenyekiti wa kijiji wakati huo alikuwa Juma Janguri (kwa sasa ni marehemu) wakanunua eneo hilo kwa Sh700,” alisema.

Chao alisema mwaka 1978 madhehebu hayo yaliacha kusali katika majengo ya shule na kuhamia katika eneo hilo kwa kusali chini ya mti kwa zamu kama ilivyokuwa katika majengo ya shule.

Alisema baadaye Wakatoliki walipata eneo lao. “Tukabaki makanisa mawili ambapo mwaka 1996 tuligawana eneo kati ya Anglikana na Lutherani, wao walibaki katika eneo hilo ambalo linavunjwa sasa,” alisema Chao.

Mwananchi: