WAZIRI WA AFYA, KUTOA TAMKO LA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HOMA YA INI DUNIANI
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,
akitoa tamko katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini
Duniani wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini
Dar es Salaam leo asubuhi. Kushoto ni Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa
Bakari Kambi.
Tamko likitolewa kwa wanahabari.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakiwa kazi wakati wa tamko hilo.
Tamko likitolewa.
Ndugu wananchi
Tarehe 28 Julai ya kila mwaka, ni siku iliyoteuliwa na Shirika la Afya
Duniani (WHO) kama siku ya Homa ya Ini (World Hepatitis Day). Lengo kuu
la maadhimisho haya ni kuielimisha na kuikumbusha jamii kutambua athari
za ugonjwa wa Homa ya Ini, jinsi ugonjwa huu unavyoambukizwa, na namna
ya kujikinga na ugonjwa huu. Ni jambo muhimu kwa nchi zote duniani
kushirikiana katika kupambana na ugonjwa huu.
Ndugu wananchi
Katika kuadhimisha Siku hii, kila mwaka Shirika la Afya Duniani hutoa
kauli mbiu yenye ujumbe maalum, unaolenga kuhamasisha na kuelimisha
jamii kuhusu madhara yanayotokana na ugonjwa huu. Kauli mbiu ya
maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani kwa mwaka huu wa 2017 ni:-
“Tokomeza Homa ya Ini” (“Eliminate Hepatitis”). Kauli mbiu hii
inatulazimu Serikali kuweka mikakati ya pamoja na wananchi ili kuweza
kudhibiti ugonjwa huu nchini na hatimaye kuweza kuutokomeza kabisa.
Ndugu wananchi
Maadhimisho haya pia yanatoa fursa ya nchi yetu kuongeza juhudi za
kutekeleza Mpango Mkakati wa kwanza wa Dunia wa Homa ya Ini (Global
Health Sector Strategy on Viral Hepatitis) kwa mwaka 2016-2021, ambao
tuliuridhia ukiwa na lengo la kuziwezesha nchi wanachama wa Shirika la
Afya Duniani kufikia lengo la kuutokomeza ugonjwa wa Homa ya Ini.
Ndugu wananchi
Ugonjwa wa Homa ya Ini ni tatizo linalohitaji juhudi za dhati kupambana
nalo. Ugonjwa huu umetajwa kuwa wa hatari na unaoua idadi kubwa ya watu
pole pole.
Kati ya watu 100, watu 8 wanaweza kuwa na maambukizi sugu ya ugonjwa huu
na wanaweza wasionyeshe dalili. Aidha, maambukizi ya ugonjwa huu ni
makubwa mara 10 zaidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na kwamba
asilimia kubwa ya wagonjwa huugundua ugonjwa huu kwenye hatua za mwisho
na hivyo kushindwa kupata matibabu mapema na kupelekea mgonjwa
kupoteza maisha.
Ndugu wananchi,
Maambukizi ya Homa ya Ini husababishwa na virusi ambavyo vinapoingia
mwilini mwa binadamu, hushambulia ini na hivyo kulifanya wakati mwingine
lisinyae na kushindwa kufanya kazi vizuri.
Katika hatua za mwishoni mwathirika wa ugonjwa huu anaweza kupata
saratani ya ini. Homa hii inaenezwa kwa njia mbalimbali kulingana na
kundi la virusi hivi. Virusi vya homa ya ini vipo katika makundi matano,
yaani A, B, C, D na E.
Pamoja na virusi hivi pia homa ya ini inaweza kusababishwa na matumizi
ya dawa kiholela, vilevi kupita kiasi, aina mbalimbali za sumu na pia
magonjwa mengine ambayo yanashambulia kinga za mwili na ini.
Uhakika wa mgonjwa kuwa na maambukizi haya hupatikana kwa kufanyiwa vipimo maalum vya kimaabara.
Ndugu wananchi
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa, vifo vitokanavyo na
Homa ya Ini vinaendelea kuongezeka. Mnamo mwaka 2015 kulikuwa na vifo
milioni 1.34 kutokana na Homa ya Ini ambavyo vilikuwa sawa na vile
vitokanavyo na Kifua Kikuu na zaidi ya vile vitokanavyo na ugonjwa wa
UKIMWI ambavyo vilikuwa milioni 1.1.
Mwaka
2015 kulikuwa na maambukizi mapya milioni 1.75 kwa watu wazima kutokana
na virusi aina ya C, hususan kutokana na matumizi ya sindano yasiyo
salama.
Ndugu wananchi,
Kwa Tanzania tafiti na takwimu chache zilizopo zinaonyesha uwepo wa
maambukizi ya virus vya Hepatitis B na C. Mfano kati ya wachangiaji damu
200,000 kwa mwaka 2016, asilimia 6 kati yao (takriban watu 12,000)
walikuwa na maambukizi ya Hepatitis B.
Aidha,
tafiti zinaonyesha kuwa, kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini Homa ya
Ini inayosababishwa na virusi vya aina B (Hepatitis B) inakadiriwa
kuwepo kwa asilimia asilimia 16-50. Kwa upande wa Homa ya Ini
inayosababishwa na virusi aina ya C (Hepatitis C) inakadiriwa kuwepo kwa
asilimia 2% miongoni mwa wanajamii.
Aidha maambukizi ya homa ya Ini ya aina ya B na C (Hepatitis B na C) ni
tatizo kubwa miongoni mwa watu wenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Ndugu wananchi
Matibabu ya Homa ya Ini ni ya gharama kubwa na ndio maana tunasema ni
bora kinga kuliko Tiba. Tiba kwa Wagonjwa waliopata kirusi aina ya A na
E, mara nyingi hutolewa kutokana na dalili zinazoambatana na ugonjwa
huu.
Kwa wagonjwa waliogundulika kuwa na Hepatitis B au C, matibabu hutegemea
hatua mgonjwa aliyofikia. Wakati mwingine magonjwa hulazimika kupewa
dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa huo kwa kipindi chote cha
uhai wake.
Gharama za dawa hizi ni kubwa sana. Kwa mgonjwa aliyepata maambukizi ya
Homa ya Ini kupitia Virusi aina ya C, gharama ya dawa ni kati ya
shilingi Milioni Tatu hadi Tano kulingana na muda wa tiba. Kupitia mradi
maalum wa awali (“Hepatitis B and C Pilot project”), matibabu kwa
wagonjwa walioathirika hapa nchini yanatolewa bila malipo katika
hospitali maalum ya Muhimbili.
Hadi sasa hakuna dawa maalum inayotumika kutibu virusi vya aina ya Hepatitis D.
Ndugu wananchi
Ugonjwa huu unaweza kukingwa kwa kutumia chanjo ambayo hutolewa kwa mtu
asiye na maambukizi ya virusi hivyo. Kwa maambukizi ya kirusi aina ya B,
chanjo ya ugonjwa huo hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi
hivyo na hutoa kinga kwa kipindi chote cha maisha yake.
Hapa nchini chanjo hii kwa sasa hutolewa kwa watoto wachanga bila
malipo. Chanjo hii ambayo ilianza kutolewa kwa watoto wachanga nchini
waliozaliwa kuanzia mwaka 2003 ipo kwenye mchanganyiko wa Pentavalenti.
Hadi kufikia mwaka 2015, inakadiriwa kuwa asilimia 97% ya watoto wote waliozaliwa kuanzia mwaka 2003 walipata chanjo hiyo.
Chanjo ya Hepatitis A ipo na inatumika kwa baadhi ya nchi lakini hapa
nchini kwetu hatujaanza utaratibu wa kutoa chanjo hiyo kwasababu tatizo
kubwa zaidi linalotukabili kwa sasa ni Hepatitis B. Hakuna chanjo dhidi
ya Hepatitis C, D na E. Hata hivyo Ugonjwa wa Hepatitis D unaweza
kuzuilika kwa kuwachanja watu dhidi ya Hepatitis B.
Ndugu wananchi,
Kama wajibu wa waajiri kuwakinga watumishi wao sehemu za kazi, chanjo ya
kuzuia maambukizi ya Hepatitis B hutolewa kwa watumishi wa sekta ya
Afya kwa gharama ya serikali. Wizara imekuwa ikiratibu utoaji wa chanjo
ya homa ya ini kwa watoa huduma za afya kwa lengo la kuwakinga watumishi
wa afya ambao wana hatari mara mbili ya kupata ugonjwa huu.
Kwanza kwa kupata maambukizi wawapo kazini katika kutekeleza majukumu
yao ya kila siku ya kutoa huduma za afya na pia wanapokuwa katika jamii
kama sehemu ya jamii. Kwa upande mwingine, sekta binafsi zina utaratibu
wao wa kugharamia chanjo kwa ajili ya kuwakinga watumishi wao sehemu za
kazi.
Ndugu wananchi
Kwa sasa Wizara inaangalia namna ya kufikia jamii iliyobaki ili kuweza
kuwapatia chanjo dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B. Wizara imeshafanya
mchanganuo rasmi ambao unaonesha kiasi cha gharama ya kununua chanjo na
vitendanishi vya vipimo vya awali, kutunza chanjo, kusambaza chanjo na
shughuli yenyewe ya uchanjaji.
Wizara pia inaangalia uwezekano wa kupata wadau kwa ajili ya
kushirikiana nao katika kazi ya kutoa chanjo hii. Kwa sasa, mtu binafsi
anayetaka kupata chanjo ya kujikinga na Hepatitis B, inabidi alipie.
Katika sekta binafsi, chanjo ya Hepatitis B inapatikana kwa shilingi
50,000 hadi 75,000 kwa mtu mmoja kwa dozi moja. Vituo vinavyotoa chanjo
hii ni pamoja na Premier Care Clinic, IST na Hindu Mandal kwa mkoa wa
Dar es salaam.
Ni matarajio yetu kuwa gharama hizi zitapungua kwa kiasi kikubwa na
kuwezesha chanjo kupatikana katika vituo vingi vya kutolea tiba hasa vya
umma baada ya uamuzi wa serikali kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa
wazalishaji ambapo bei ya chanjo ya Homa ya Ini katika Bohari ya Dawa
(MSD) sasa inauzwa shillingi 5,300 kutoka shillingi 22,000.
Ndugu wananchi
Hatua zinazofanyika na Wizara katika kudhibiti Homa ya Ini ni pamoja na :-
1.
Kuunda kikosi kazi cha Taifa kinachojumuisha wataalam kutoka taasisi
mbalimbali. Kikosi kazi hiki kimepewa jukumu la kuandaa Mpango Mkakati
wa Taifa wa Kudhibiti na Kutokomeza Ugonjwa wa Homa ya Ini nchini. Aidha
kamati hii inakamilisha Mpango Mkakati wa kudhibiti ugonjwa wa Ini
nchini wa 2017-2021
2.
Kuandaa vielelezo vinavyohusu ugonjwa wa Homa ya Ini (Viral Hepatitis),
ili kuuelimisha umma juu ya ugonjwa huu na namna gani maambukizi
yanaweza kuzuiwa.
3. Kuendelea kutoa chanjo kwa watumishi wa afya ambapo katika mwaka 2015
Wizara ilinunua dozi zaidi ya 650,000 ya chanjo dhidi ya Hepatitis B
kwa ajili ya kuwachanja watumishi walio katika mazingira hatarishi na
chanjo hiyo imekwishasambazwa katika mikoa yote.
4. Aidha, Wizara inakamilisha
mipango ya uwezekano wa kuhakikisha chanjo hii ya Hepatitis B
inapatikana kwa watu wote wanaohitaji na kwa gharama nafuu.
Ndugu wananchi,
Kwa sasa hakuna ushahidi wa mlipuko wa homa ya ini nchini. Hata hivyo,
wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki wapo katika hatari ya kupata
maambukizi ya ugonjwa huu, hususan Hepatitis B na C, kuliko aina
nyingine, yaani A, D na E kutokana na kuwa njia za maambukizi ya Virusi
vya aina ya B na C hufanana kwa kiasi kikubwa na zile za maambukizi ya
VVU.
Leo tunapoadhimisha Siku ya Homa ya Ini, na ili tuweze kwenda sambamba
na mataifa mengine duniani na katika kufanikisha Ajenda ya Maendeleo
Endelevu ifikapo mwaka 2030, Msisitizo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni kwa wananchi na wadau wote kuendelea
kuona umuhimu na kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa
Homa ya Ini hususan kwa kutumia fursa zilizopo na kuwekeza katika
mapambano dhidi ya ugonjwa huu.
Naomba nihitimishe kwa kuwataka wafanyakazi wa Mpango wa Damu Salama
kuendelea na kazi nzuri ya kupima damu zote za wachangiaji, kuwataka
wafanyakazi wa sekta ya afya kuzingatia kanuni za usalama, kuwashauri
jamii kuepuka na kujidunga madawa ya kulevya, kuepuka ngono zembe, na
mwisho kabisa kuwaomba wadau wote kushirikiana na Serikali katika juhudi
za kuondoa ugonjwa wa Homa ya Ini hapa nchini.