Zinazobamba

“WATANZANIA TUACHE KUTUMIA DOMAIN ZA .COM”- ENG. NGONYANI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani amewataka Watanzania kuachana na matumizi ya vikoa (domain) tofauti na .tz.
Enj. Ngonyani ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano ambao unajadili namna ya kushirikiana kukuza matumizi ya vikoa kwa wananchi kwa nchi mbalimbali ambazo zimeshiriki mkutano huo.
Naibu Waziri huyo alisema matumizi ya Watanzania wanaotumia kikao cha .tz ni ndogo kulinganisha na idadi ya watumiaji wa mitandao nchini hivyo wabadilike kwani kwa kutumia vikoa tofauti na .tz wanazifaidisha nchi zinamiliki hivyo vikoa.
“Sisi Tanzania tupo nyuma sana inawezekana ni kwasababu mambo mengi hatuelewi tumezoea kutumia .com, hotmail, gmail lakini hizo sio zetu ni za Wamarekani au Waingereza ni wakati umefika sasa na sisi tuna uwezo wa kutengeneza rajisi yetu,
“Tuwahamasishe Watanzania kuwa waachane na matumizi ya .com, yahoo, hotmail na kadhalika sababu tunawanufaisha mataifa ya nje, katika kila huduma unayotumia katika mitandao ile mataifa ya nje ndiyo yananufaika,” amesema Mhandisi Ngonyani na kuongeza.
“Faida kubwa kwa kutumia kikoa cha Tanzania ni kwamba mtu akiwa Australia anawasiliana na wewe akiona unatumia .tz anajua upo Tanzania lakini ukitumia .com hawezi kujua upo wapi, ukiwa unaagiza vitu kutoka nje ukitumia .tz inakusaidia sana kukutambulisha kuwa wewe ni Mtanzania, inakupa uaminifu, inampa mtu imani kuwa huyu ni mtu sahihi na yupo Tanzania.”
Nae Makamu wa Rais wa AfTLD, Alli Hadji Mmadi alisema matumizi ya kikoa kwa Afrika bado ni madogo kulinganisha na idadi ya watu waliopo na hivyo kuwataka watu wote ambao wanatumia mitandao kuhakikisha wanatumia kikao cha .tz.
“Kwanini usitumie kikao cha .tz na wakati kinakutambulisha wewe unatokea sehemu gani, matumizi ya vikoa Afrika bado ni madogo sana na hilo ni changamoto, kati ya watu bilioni ni watu milioni 2.9 tu ndiyo wanatumia vikoa vya nchi zao, tuna kazi ya kuhakikisha idadi inaongezeka,” amsema Mmadi.
Kwa upande wa Mkurugenzi mtendaji wa .tz Registry, Abibu Ntahigiye amesema huo ni mkutano wa tano kufanyika na kupitia mkutano huo wataweza kuzungumza ni namna gani wanaongeza idadi ya watumiaji wa vikoa vya Afrika.