“WANAWAKE MILIONI 214 DUNIANI HAWATUMII NJIA ZA UZAZI WA MPANGO”- UNFPA
Ikiwa imesalia siku moja kabla ya kufikia Siku ya
Idadi ya Watu Dubniani, Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia Idadi ya
Watu (UNFPA) limetoa taarifa kwa wananchi kuhusu siku hiyo.
Akisoma taarifa kwa
niaba ya Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Dk. Hashina Begum alisema idadi ya watu duniani
imekuwa ikiongezeka na wanaoathirika zaidi ni wanawake na sababu kubwa ikiwa ni
kutotumia uzazi wa mpango.
“Kila siku wanawake
waliopo katika mazingira hatarishi na hasa masikini na wakimbizi wanakumbana na
changamoto za kijamii, kiuchumi na kijografia zinazosababisha kukosa huduma za
mpango wa uzazi … pamoja na hatua kubwa ziliyopigwa wanawake milioni 214 katika
nchi ambazo zinaendelea hawatumii njia yoyote ya uzazi wa mpango na
wengi wao wanaishi katika nchi 69 ambazo ni masikini,
“Afya ya uzazi wa mpango
iiliyo nzuri inaweza kukuka uchumi na kuchangia maendeleo endelevu kwa kuwapa
wanawake fursa ya kumaliza elimu na kuwa sehemu ya nguvu kazi ya kuchangia pato
la familia na taifa kwa ujumla,” alisema Hashina.
Aidha Dk. Hashina
alizungumza kuhusu mipango ya UNFPA wa kukabiliana na ongezeko la watu kwa
kutumia njia ya uzazi wa mpango, “Uzazi wa mango ni lengo namba moja la malengo 17 ya
maendeleo endelevu (SDGs) la kumaliza umasikini, shirika limejipanga
kuhakikisha changamoto za ukosefu wa afya ya uzazi wa mpango zinaisha mwaka
2030.”
Naye Mratibu wa
Dawa za Uzazi wa Mpango kutoka Wizara ya Afya, Dk. Cosmas Swai alisema kitaifa
siku ya Idadi ya Watu Duniani itafanyika katika viwanja vya Mwembeyanga
vilivyopo Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam na huduma mbalimbali kuhusu uzazi
wa mpango zitakuwa zikitolewa na Wizara ya Afya, UNFPA na taasisi zingine
zisizo za kiserikali.