UTAPIAMLO BADO TATIZO SUGU NCHINI,SOMA HAPO KUJUA
NA KAROLI VINSENT
UTAPIAMLO umetajwa kama moja ya matatizo sugu ya kiafya nchini yanayoathiri makundi yaliyohatarini kama vile watoto wachanga, watoto wadogo na wanawake waliofikisha umri wa kushika ujauzito.
Hayo yalibainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mtaamu wa Chakula na Afya ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) Profesa Theobald Mosha katika mkutano wa kufunga Mradi wa Masava (Mafuta Asili ya Alizeti ya Vitammini A).
“Utapiamlo ni changamoto kubwa ya maendeleo nchini Tanzania, lakini mradi uliohusisha wadau mbalimbali umesaidia kulishughulikia suala hili kwa kuyafanya mafuta ya kupikia yenye vitamin A yapatikane kwa wingi ili kukabiliana na tatizo hilo,” alisema Profesa Moshi.
Alisema katika maeneo mengi ya vijijini milo inakosa virutubisho vya msingi kwa ajili ya kujenga kinga thabiti ya mwili ili kuwa na afya bora na kupambana na magonjwa hususani kwa wanawake na watoto.
Profesa Mosha alibainisha kuwa katika muongo uliopita watoto wanaokadiriwa kufikia 600,000 walio chini ya miaka mitano walifariki nchini kutokana na upungufu wa virutubisho vya lishe.
Alieleza kwamba changamoto kubwa ni upungufu wa vitamin A ambapo alisema ni kwa robo tatu ya watoto walio chini ya miaka mitano na asilimia 37 ya wanawake wanye uumri wa miaka 15 hadi 49 wanaosumbuliwa na tatizo la upungufu wa vitamin A.
Mradi huo wa miaka mitatu uliokuwa chini ya shirika la Mennonite Economic Development Associates (MEDA), Chuo Kikuu cha Waterloo na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) wamethibitisha tatizo la upungufu wa virutubisho vya vitamin A linaweza kutatuliwa kwa kutumia kwa kutumia mafuta yaliyoongezwa virutubisho ambayo ndiyo hayo maalumu ya MASAVA.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Ulisubisya Mpoki alisema mradi huo upo katika ajenda kubwa ya lishe nchini ambapo alieleza serikali inaendelea kuweka msisitizo juu ya suala hilo.
Aidha alisema licha ya kupiga hatua katika kuliboresha suala hilo bado mamilioni ya wanawake na watoto wanaendelea kuteseka na aina mbalimbali za lishe duni. Alisema mradi wa mafuta hayo yenye vitamin A unaendana na ajenda ya kitaifa ya kulichunguza tatizo hilo sugu kwa jicho la kiubunifu na kwa wigo mpana.
Alisema serikali imeweka nia kikamilifu kwa ajili ya fumbuzi za kibunifu za suala la utapia mlo na usalama wa chakula iliyosisitizwa kupitia mpango wa scaling up Nutrition.